Mtunzi  (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kushirikisha katika ´ibaadah ya Allaah (Ta´ala).”

Utambulisho wa ´ibaadah:

´Ibaadah ni yale maamrisho na makatazo yote yaliyokuja katika Shari´ah. Yale yote yaliyoamrishwa na Shari´ah, ni mamoja iwe ni maamrisho ya uwajibu au maamrisho ya yanayopendeza, au imeyakataza, ni mamoja iwe ni makatazo ya uharamu au makatazo ya kuchukiza. Maamrisho ikiwa ni kwa njia ya ulazima, basi ni lazima kuyatekeleza, na ikiwa ni kwa njia ya kupendeza basi itapendeza kuyafanya. Kadhalika inapokuja katika makatazo, ikiwa ni makatazo ya uharamu ni wajibu kuyaacha na ikiwa ni makatazo ya kuchukiza basi inachukiza kuyafanya.

Vilevile unaweza kusema ´ibaadah ni jina lililokusanya kila ambacho Allaah anakipenda na kukiridhia, sawa katika maneno au matendo, ya ndani na ya nje[1].

Kwa hivyo ´ibaadah ni kila amrisho au katazo lililokuja katika Shari´ah. Kwa mfano swalah ni ´ibaadah. Zakaah ni ´ibaadah. Swawm ni ´ibaadah. Hajj ni ´ibaadah. Kuweka nadhiri ni ´ibaadah. Kuchinja ni ´ibaadah. Du´aa ni ´ibaadah. Kutegemea ni ´ibaadah. Shauku ni ´ibaadah. Woga ni ´ibaadah. Kupigana Jihaad katika njia ya Allaah ni ´ibaadah. Kuamrisha mema na kukataza maovu ni ´ibaadah. Kuwafanyia wema majirani ni ´ibaadah. Kuwaunga ndugu ni ´ibaadah. Vivyo hivyo makatazo. Muislamu anatakiwa kuacha makatazo kwa ajili ya kumwabudu Allaah. Anatakiwa kuacha shirki, kuacha kuua watu, kushambulia mali zao, kukiuka heshima zao na pia kukanusha haki. Anafanya ´ibaadah kwa kuacha maovu haya ikiwa ni pamoja vilevile na uzinzi, kunywa pombe, kuwaasi wazazi wawili, kusengenya, kueneza uvumi na kula ribaa. Yote haya ni ´ibaadah.

Kwa hiyo ´ibaadah ni maamrisho na makatazo. Inapokuja katika maamrisho unayafanya. Na inapokuja katika makatazo unayaacha. Yote mawili kwa ajili ya kumwabudu Allaah (´Azza wa Jall).

[1] Majmuu´-ul-Fataawaa (10/149).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tabswiyr-ul-Anaam bisharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 14-15
  • Imechapishwa: 09/04/2023