6 – Zayd bin al-Hubaab ametuhadithia, kutoka kwa ´Aliy bin Mas´adah: Qataadah ametueleza: Anas bin Maalik ametueleza ya kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Uislamu uko waziwazi na imani ni ndani ya moyo.” Kisha akaashiria namna hii kwa mkono wake na kusema: ”Uchaji Allaah uko hapa. Uchaji Allaah uko hapa.”[1]

7 – Musw´ab bin al-Muqdaam ametuhadithia: Abu Hilaal ametueleza, kutoka kwa Anas ambaye amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hana imani yule ambaye hana amana.”[2]

8 – Abu Usaamah ametuhadithia: ´Awf bin ´Abdillaah bin ´Amr bin Hind al-Jamaliy ametueleza kwamba ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Imani huanza moyoni kama doa jeupe. Kila ambavyo imani inaongezeka, ndivo huongezeka weupe huo mpaka moyo mzima unakuwa mweupe. Unafiki huanza moyoni kama doa jeusi. Kila ambavyo unafiki unaongezeka, ndivo huongezeka weusi huo mpaka moyo mzima unakuwa mweusi. Naapa kwa Ambaye nafsi yangu iko mkononi Mwake! Lau mtaufungua moyo wa muumini, basi mtamkuta ni mwenye moyo mweupe, na lau mtaufungua moyo wa mnafiki, basi mtaukuta ni mwenye moyo mweusi.” 

9 – Wakiy´ ametuhadithia: al-A´mash ametueleza, kutoka kwa Sulaymaan bin Masiyrah, kutoka kwa Twaariq bin Shihaab ambaye ameeleza kuwa ´Abdullaah amesema:

“Wakati mtu anapotenda dhambi, basi anawekwa moyoni mwake doa jeusi. Kisha anatenda dhambi nyingine ambapo akaweka jingine mpaka rangi ya moyo wake ikawa kama rangi ya mwana kondoo wa rangi ya majivu.”[3]

10 – Wakiy´ ametuhadithia, kutoka kwa Sufyaan: Hishaam amesimulia kutoka kwa baba yake ambaye amesema:

“Haupungui uaminifu wa mja isipokuwa imani yake pia hupungua.”

11 – Sufyaan bin ´Uyaynah ametuhadithia, kutoka kwa ´Amr, kutoka kwa ´Ubayd bin ´Umayr ambaye amesema:

“Imani ni heshima.”[4]

[1] Cheni ya wapokezi wake ni dhaifu kwa sababu ya  ´Aliy bin Mas´adah ambaye alikuwa na kumbukumbu dhaifu. ´Abdul-Haqq al-Ishbiyliy amesema:

“Hadiyth haikuhifadhiwa.” (al-Ahkaam (10))

[2] Hadiyth ni Swahiyh na cheni ya wapokezi ni nzuri. Ahmad ameipokea kupitia njia nyingine, kutoka kwa Abu Hilaal. Ameipokea tena kupitia njia nyingine kutoka kwa Anas. Ibn Hibbaan ameipokea kupitia njia nyingine ya tatu kutoka kwake. Zote zina ziada:

“… na hana imani yule ambaye hana uaminifu.”

[3] Cheni ya wapokezi ni Swahiyh.

[4] Bi maana waumini wanaheshimiwa. Watu wanawaheshimu waumini kwa sababu wanatukuzwa na kumuogopa Allaah (Ta´ala). Tafsiri nyingine ni kwamba waumini wanayaheshimu maasi kwa sababu wanayaepuka. Tazama ”an-Nihaayah”.

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 18-19
  • Imechapishwa: 06/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy