Lengo la nne: Kutekeleza kumdhukuru Allaah

Miongoni mwa malengo ya hajj ni kutekeleza kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Bali matendo yote ya Kishari´ah yamewekwa kwa ajili yake. Hajikurubishi mwenye kujikurubisha kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa mfano wake. Swalah imewekwa katika Shari´ah kwa ajili ya kumdhukuru Allaah:

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي

“Simamisha swalah kwa ajili ya kunidhukuru.”[1]

Hajj, swawm na matendo ya kitiifu yote yamewekwa katika Shari´ah kwa ajili ya kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ

“Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafah, mtajeni Allaah al-Mash´ar al-Haraam.”[2]

Kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) ni miongoni mwa malengo ya hajj. Bali hajj na matendo ya kitiifu mengine yamewekwa katika Shari´ah kwa ajili ya kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall). Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kama ilivyotajwa katika “al-Musnad” ya Imaam Ahmad na vitabu vyenginevyo kupitia kwa mama wa waumini ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa):

“Kutufu katika Nyumba, Swafaa na Marwah na kurusha mawe katika nguzo vimewekwa kwa ajili ya kutekeleza kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall).”[3]

Kutaja kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) matendo haya matatu; Twawaaf,  Sa´y na kurusha mawe sio kwa njia ya kukomeka. Bali ni kwa njia ya kupigia mfano. Kwa sababu matendo yote ya hajj yamewekwa kwa ajili ya kutekeleza kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala).

Kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) ndio kitendo kitukufu zaidi na utiifu mkubwa zaidi. Kwa ajili hii amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Je, nisikujuzeni bora ya matendo yenu, kitakasifu zaidi mbele ya Mfalme wenu, kilicho juu zaidi katika ngazi zenu, ambacho ni bora zaidi kwenu kuliko kutoa dhahabu na fedha, ambacho ni bora kwenu kuliko kukutana na maadui wetu mkazikata shingo zao na wao wakazikata shingo zenu?” Wakasema: “Ndio.” Akasema: “Kumdhukuru Allaah (Ta´ala).”[4]

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَذِكْرُ اللَّـهِ أَكْبَرُ

“Hapana shaka kumdhukuru Allaah ni kubwa zaidi.”[5]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا

“Enyi walioamini!  Mdhukuruni Allaah kwa wingi wa kumdhukuru na msabihini asubuhi na jioni.”[6]

وَالذَّاكِرِينَ اللَّـهَ كَثِيرًا وَالذَّاكِرَاتِ أَعَدَّ اللَّـهُ لَهُم مَّغْفِرَةً وَأَجْرًا عَظِيمًا

”… wanaume na wanawake wanaomdhukuru Allaah kwa wingi wanaume, basi Allaah amewaandalia msamaha na ujira mkubwa.”[7]

Kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) ni utiifu mkubwa na ´ibaadah tukufu ambayo inatakiwa kuwa pamoja na mja katika hajj yake wakati wa swalah yake, kufunga kwake na katika utiifu wake wote. Kwa sababu watu walio na thawabu nyingi inapokuja katika mambo ya utiifu ni wale wanaomdhukuru Allaah kwa wingi. Imaam Ahmad na at-Twabaraaniy wamepokea kupitia kwa Mu´aadh bin Anas al-Juhaniy (Radhiya Allaahu ´anh) ambaye amesimulia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba kuna mtu alimuuliza kwa kusema:

“Ni mapambano yepi yaliyo na thawabu nyingi?” Akasema: “Ni wale wanaomdhukuru Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kwa wingi.” Akauliza tena: “Ni wafungaji wepi walio na thawabu nyingi?” Akasema: “Ni wale wanaomdhukuru Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kwa wingi.” Kisha akatutajie wenye kuswali, wenye kutoa zakaah na wenye kutoa swadaqah ambapo wote hao Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisema: “Ni wale wanaomdhukuru Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) kwa wingi.”

Abu Bakr (Radhiya Allaahu ´anh) alisema kumwambia ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh): “Ee Abu Hafswah! Wanaomdhukuru Allaah wameenda na kila kheri.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ajal.”[8]

´Allaamah Ibn-ul-Qayyim amesema:

“Wabora wa kila matendo ni wale wanaomdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) kwa wingi. Wabora wa wenye kufunga ni wale  wanaomdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) kwa wingi katika funga zao. Wabora wa wenye kutoa swadaqah ni wale  wanaomdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) kwa wingi. Wabora wa mahujaji ni wale  wanaomdhukuru Allaah (´Azza wa Jall) kwa wingi. Vivyo hivyo matendo yaliyobaki.”[9]

Kwa hiyo mahujaji hawawi katika ngazi moja na hawawi katika thawabu wanazopata. Kwa sababu wako katika wao ambao wanakithirisha kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall), wako wanaofanya hivo kati na kati, wako wanaofanya hivo kidogo, wako wanaoghafilika na wenye kupuuza. Msaada ni wenye kuombwa kutoka kwa Allaah.

Inapasa kwa mahujaji kuchunga wakati wao katika hajj zao na kupupia kumdhukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) kwa wingi, kusoma Qur-aan, kuleta Talbiyah, kusema “Subhaan Allaah”, “Alhamdulillaah”, kusoma vitabu vya kielimu na mfano wa hayo. Lengo ni kuzifanya nyingi na kubwa thawabu zao katika hajj zao ili waweze kufuzu thawabu tukufu.

[1] 20:14

[2] 02:198

[3] Ahmad (24351).

[4] at-Tirmidhiy (3377).

[5] 29:45

[6] 33:41-42

[7] 33:35

[8] Ahmad (15614), “al-Mu´jam al-Kabiyr” ya at-Twabaraaniy (20/186) nambari (407). Ni Hadiyth nzuri kwa sababu ina zenye kuitolea ushahidi.

[9]  al-Waabil as-Swayyib, uk. 181.

  • Mhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Maqaaswid-ul-Hajj, uk. 19-24
  • Imechapishwa: 16/08/2018