04 – Kujifunza elimu ya dini

Ee mwanafunzi wa kike! Isiwe lengo lako la kusoma ni kupata cheti tu, bali lengo lako iwe ni kutafuta radhi za Allaah ambazo kwazo utapata radhi za Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Jengine ni kwamba nakusisitiza usitosheke na vitabu vya shule peke yake, bali pupia pia kusoma vitabu vingine vya wanavyuoni. Kwani mwanamke ambaye anajifunza elimu ya dini anayo hadhi kubwa. Amesema (Ta´ala):

يَرْفَعِ اللَّـهُ الَّذِينَ آمَنُوا مِنكُمْ وَالَّذِينَ أُوتُوا الْعِلْمَ دَرَجَاتٍ

“Allaah atawainua wale walioamini miongoni mwenu na waliopewa elimu daraja za juu.”[1]

أَفَمَن يَعْلَمُ أَنَّمَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِن رَّبِّكَ الْحَقُّ كَمَنْ هُوَ أَعْمَىٰ ۚ إِنَّمَا يَتَذَكَّرُ أُولُو الْأَلْبَابِ

“Je, anayejua kwamba yaliyoteremshwa kwako kutoka kwa Mola wako ni haki [na akayafuata je analingana] kama aliyekuwa kipofu? Hakika wanazingatia wenye akili tu.”[2]

إِنَّمَا يَخْشَى اللَّـهَ مِنْ عِبَادِهِ الْعُلَمَاءُ

“Hakika si venginevo wanaomkhofu Allaah miongoni mwa waja Wake ni wanazuoni.”[3]

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Yeyote ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa ufahamu katika dini.”[4]

”Yule anayeshika njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah humsahilishia kwayo njia ya kuelekea Peponi.”[5]

Inastahiki kwa mwanamke wa Kiislamu kupatiliza njia zote zinazofikisha kwenye elimu hali ya kukusudia kwa jambo hilo uso wa Mola wake; Amnataka Allaah na Pepo, anataka kuifahamu dini, anataka kumwabudu Allaah kwa utambuzi na ubainifu na pia kuwaokoa watu kwa elimu yake.

Inatosha kuhusu fadhilah za elimu, dada yangu wa Kiislamu, ya kwamba kadri mtu anavyoongezeka elimu yake ndivyo inazidi khofu yake kwa Allaah. Pia inatosha ya kwamba wanazuoni ndio warithi wa Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam). Kwa hivyo ni inakulazimu kujifunza elimu ili uweze kuifikia fadhilah hii kuu.

[1] 58:11

[2] 13:19

[3] 35:28

[4] al-Bukhaariy na Muslim.

[5] at-Tirmidhiy. Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy. Tazama ”Swahiyh-ul-Jaamiy´” (02/1079) nr. 2698.

  • Muhusika: Dr. ´Abdul-´Aziyz bin Daawuud al-Faaiz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Tawjiyhaat wa Tanbiyhaat lil-Fataati al-Muslimah, uk. 12-13
  • Imechapishwa: 27/01/2026