Imaam ´Abdul-Ghaniy bin ´Abdil-Waahid al-Maqdisiy (Rahimahu Allaah) amesema:

197 – ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) amesema:

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”[1]

Ameipokea Abu Daawuud na akasema:

“Hili linahusu katika nadhiri tu. Vilevile ndio maoni ya Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah).”

Hadiyth hii ni tukufu. Inafahamisha ya kwamba mwenye kufa ilihali anadaiwa funga basi imesuniwa kwa wale mawalii wake ambao ni wale jamaa zake. Imesuniwa kwao kumfungia. Kwa mfano akafa baada ya kuweka nadhiri, swawm ya kafara au deni la Ramadhaan ambalo hakufunga ilihali anaweza kufunga. Lakini akachukulia wepesi na akachelewesha kulipa, basi ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa wale jamaa zake kumfungia. Nao ni wale watoto wake, ndugu zake au jamaa zake wengine kama vile wake zake. Itasihi pia akifungiwa na wasiokuwa jamaa zake kwa sababu ni deni. Deni la Allaah lina haki zaidi ya kutekelezwa. Deni linalipwa na jamaa na wasiokuwa jamaa. Lakini jamaa zake ndio wenye haki zaidi na bora zaidi. Kwa sababu kufanya hivo ni kumtendea wema na kuunga kizazi chake. Lisipokuwa wepesi suala la kumfungia basi atatolewa chakula kumpa masikini kwa kila siku iliyompita.

Kuhusu maneno ya Abu Daawuud kutoka kwa Ahmad kwamba inahusu nadhiri peke yake ni maoni dhaifu. Maoni ya sawa ni kwamba ni yenye kuenea inahusu nadhiri na Ramadhaan. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) amesema kwa kuenea:

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Hapa ni kwa njia ya kuenea na hivyo kunaingia aina zote za swawm ambazo ni lazima. Imekusanya swawm za kafara, za nadhiri na ya Ramadhaan. Hadiyth inakusanya zote. Hivyo basi, haijuzu kuifanya maalum kwa nadhiri peke yake isipokuwa kwa dalili, kitu ambacho hakipo. Imethibiti katika Hadiyth ya Ibn ´Abbaas katika Musnad ya Ahmad aliyepokea kwamba kuna mwanamke aliyesema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika mama yangu amefariki na anadaiwa swawm ya Ramadhaan. Je, nimfungie?” Akasema: “Je, waonaje kama mama yako angelikuwa na deni ungemlipia?” Mlipie deni lake analodaiwa na Allaah. Hakika Allaah ana haki zaidi ya kulipwa.”[2]

Waulizaji walikuwa wakija na kumuuliza (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) ambapo mmoja wao anasema:

“Ee Mtume wa Allaah! Hakika mama yangu amefariki na anadaiwa funga ya mwezi.”[3]

Mwingine anakuja na kusema:

“Hakika mama yangu amefariki na anadaiwa funga ya miezi miwili.”[4]

Mwingine anakuja na kusema:

“Hakika mama yangu amefariki na anadaiwa funga kadhaa.”[5]

Mtume anawaamrisha kulipa na hapambanui kile wanachomuuliza kama ni Ramadhaan. Kama ingelikuwa inahusu nadhiri peke yake basi (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) angelipambanua. Wakati alipotoa fatwa ya kuenea basi ikafahamisha juu ya kuenea. Kwa ajili hiyo amesema (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam):

“Mwenye kufa na juu yake yuko na swawm basi afungiwe na walii wake.”

Hii imeenea. Ni sentesi yenye kuenea na imekusanya aina zote za funga ya lazima; swawm ya nadhiri, swawm ya kafara au swawm ya Ramadhaan. Isipokuwa ambaye aliacha kufunga Ramadhaan kutokana na udhuru akiwa amekula kutokana na maradhi na akafa ndani ya ugonjwa wake huo au amekula kutokana na safari na akafa ndani ya safari yake hiyo, basi huyu amepewa udhuru au alipona lakini hakuishi kiasi cha zile siku alizokuwa anadaiwa. Mtu kama huyu atafungiwa kiasi cha zile siku zilizomkuta akiwa mzima. Akifungiwa mwezi mzima ni vizuri na hakuna neno. Lakini haitolazimika kumfungia isipokuwa ikiwa kama alizembea baada ya kupona kutoka katika maradhi yake na akapuuza na yakampita masiku kwa kiwango cha masiku anayodaiwa na asifunge. Lakini akiwa amefariki ndani ya maradhi yake ni mwenye kupewa udhuru.

[1] al-Bukhaariy (1952) na Muslim (1147).

[2] Ahmad (1970).

[3] al-Bukhaariy (1953) na Muslim (1148).

[4] al-Bazzaar (5004).

[5] Ibn Maajah (1759). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah” (1424).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ifhaam fiy Sharh ´Umdat-il-Ahkaam (01/405-407)
  • Imechapishwa: 21/03/2022