Mlinganizi anapasa kuwa na utambuzi juu ya kile anachokilingania. Awe na elimu sahihi inayotokana na Qur-aan na Sunnah. Kila elimu ambayo inachukuliwa kutoka katika visivyokuwa hivyo viwili ni lazima kwanza kuipima juu ya Qur-aan na Sunnah. Baada ya kuipima ima iwe yenye kuafikiana au yenye kwenda kinyume navyo. Ikiwa ni yenye kuafikiana basi itakubaliwa. Ikiwa ni yenye kwenda kinyume navyo basi italazimika kuirudisha kwa mwenye nayo pasi na kujali ni nani. Imethibiti kwamba Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mawe yanakaribia kukushukieni kutoka mbinguni. Mimi nasema “Mtume wa Allaah amesema” nanyi mnasema “Abu Bakr na ´Umar wamesema.”

Hali ikiwa ndio hii juu ya maneno ya Abu Bakr na ´Umar ambayo yanapingana na maneno ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), tusemeje juu ya maneno ya wasiokuwa hao wawili inapokuja katika elimu, kumcha Allaah, uswahaba na ukhalifa? Hakika kuyarudisha maneno yake pale yanapokwenda kinyume na Qur-aan na Sunnah kutakuwa kuna haki zaidi. Amesema (Ta´ala):

فَلْيَحْذَرِ الَّذِينَ يُخَالِفُونَ عَنْ أَمْرِهِ أَن تُصِيبَهُمْ فِتْنَةٌ أَوْ يُصِيبَهُمْ عَذَابٌ أَلِيمٌ

“Basi watahadhari wale wanaokwenda kinyume amri yake; isije kuwapata fitina au ikawapata adhabu iumizayo.”[1]

Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Unajua ni nini fitina? Fitina ni shirki. Labda akirudisha baadhi ya maneno yake kukaingia moyoni mwake kitu katika upindaji na hivyo akaangamia.”

Zawadi ya kwanza anayotakiwa kuwa nayo anayelingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) ni kwamba awe na elimu inayotokana na Kitabu cha Allaah na Sunnah Swahiyh na yenye kukubalika kutoka kwa Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Ama kufanya ulinganizi pasi na elimu ni ulinganizi uliojengeka juu ya ujinga. Ulinganizi unaotokana na ujinga madhara yake ni makubwa zaidi kuliko manufaa yake. Kwa sababu mlinganizi huyu ameshaiteua nafsi yake kama mwongozaji na mwelekezaji. Kwa hivyo akiwa ni mjinga, basi atakuwa ni mpotofu na mwenye kupotosha. Aidha ujinga wake huu unakuwa wenye kupandiana. Ujinga wenye kupandiana ni mbaya zaidi kuliko ujinga mwepesi. Ujinga mwepesi unamzuia mwenye nao na wala hazungumzi. Isitoshe ujinga mwepesi unaweza kuondoshwa kwa kusoma. Lakini tatizo kubwa ni pale ambapo ujinga unakuwa wenye kupandiana. Huyu ambaye ana ujinga uliopandiana hatonyamaza. Bali atazungumza japo ni kwa ujinga. Hapo ndipo atakuwa muharibifu zaidi kuliko atavyoangaza.

[1] 24:63

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 28/10/2021