03. Sababu ya pili ya maisha mazuri: Kuishi vizuri na kila mtu

2- Miongoni mwa sababu zinazoondosha msongo wa mawazo, misononeko na kutokuwa na amani ni kuwatendea wema watu kwa maneno na vitendo na aina mbalimbali za wema. Yote hayo ni katika kheri na wema. Allaah humwondoshea mwema na muovu misononeko na masikitiko kwa kwa kiasi cha vile mtu atayatendea kazi. Lakini inapokuja katika mambo hayo muumini anakuwa na fungu kubwa zaidi. Yeye anapambanuka na wengine kwa njia ya kwamba wema wake unatokana na kumtakasia nia Allaah na kutarajia thawabu kutoka Kwake. Hivyo Allaah anamfanyia wepesi wa kutenda wema kutokana na ile kheri anayotaraji. Sambamba na hilo Allaah anamwondoshea yale mambo yenye kuchukiza kwa sababu ya nia yake safi na kutaraji kwake malipo. Amesema (Ta´ala):

لَّا خَيْرَ فِي كَثِيرٍ مِّن نَّجْوَاهُمْ إِلَّا مَنْ أَمَرَ بِصَدَقَةٍ أَوْ مَعْرُوفٍ أَوْ إِصْلَاحٍ بَيْنَ النَّاسِ ۚ وَمَن يَفْعَلْ ذَٰلِكَ ابْتِغَاءَ مَرْضَاتِ اللَّـهِ فَسَوْفَ نُؤْتِيهِ أَجْرًا عَظِيمًا

“Hakuna kheri katika minong’ono yao mingi isipokuwa anayeamrisha swadaqah au mema au kusuluhisha kati ya watu. Na yeyote atakayefanya hivyo hali ya kutaka radhi za Allaah, basi tutampa malipo makubwa.”[1]

Akaeleza (Ta´ala) kwamba mambo haya yote ni yenye kheri pasi na kujali yametoka kwa nani. Siku zote kheri inavuta kheri zengine na pia inazuia shari na kwamba muumini anayetaraji malipo Allaah humpa thawabu kuu. Miongoni mwa thawabu hizo kuu ni kuondoshewa msongo wa mawazo, misononeko, shida na mambo mfano wake.

[1] 04:114

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 08/06/2020