2 – Kipengele cha pili: Majina ya Allaah hayakufupika kwa idadi maalum

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Hadiyth iliyoshuhurika:

“Nakuomba kwa kila jina ambalo ni Lako ulilojiita Mwenyewe au ukaliteremsha ndani ya Kitabu Chako na ukamfunza mmoja katika viumbe Wako au ukalificha katika elimu iliyofichikana huko Kwako.”[1]

Haiwezekani kuyafanyia kikomo wala kuyazunguka yale ambayo Allaah ameyaficha katika elimu Yake iliyofichikana Kwake. Haya yanaoanishwa na maneno yake katika Hadiyth Swahiyh isemayo:

”Hakika Allaah anayo majina tisini na tisa. Yule atakayeyadhibiti ataingia Peponi.”[2]

Maana ya Hadiyth ni kwamba miongoni mwa majina ya Allaah ni yale tisini na tisa na yule atakayeyadhibiti ataingia Peponi. Makusudio sio kuyafupisha majina ya Allaah katika idadi hii. Mfano wa hilo ni kama mtu aseme kuwa yuko na pesa tisini na tisa ambazo ameziandaa kwa ajili ya kuzitoa swadaqah. Hiyo haina maana kwamba kuna uwezekano ukawa na pesa zingine ulizoziandaa kwa kazi nyingine isiyokuwa swadaqah.

[1] Ahmad (01/391, 452) na Ibn Hibbaan (2372). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”as-Swahiyhah” (199).

[2] al-Bukhaariy (6410), Muslim (2677) na Ibn Maajah (3860).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ta´aliyq mukhtaswar ´alaa Lum´at-il-I´tiqaad, uk. 22-23
  • Imechapishwa: 06/10/2022