03. Lengo la Maswahabah kuendelea kulingania na kupambana

Maswahabah zake baada yake wakaibeba amana na wakapita juu ya njia. Hivyo wakalingania katika dini ya Allaah (´Azza wa Jall) na ulimwenguni kote wakaenea walinganizi wa haki na wapambanaji katika njia ya Allaah (´Azza wa Jall). Hawakuwa wenye kuchelea kwa ajili ya Allaah lawama za wenye kulaumu. Walikuwa wanafikisha Ujumbe wa Allaah, wanamwogopa na wala hawakuwa wanamwogopa yeyote isipokuwa Allaah (Jalla wa ´Alaa). Basi wapiganaji na wapambanaji wakaenea ulimwenguni kote, walinganizi wenye kuongoza na wema wenye kutengeneza ambao walikuwa wakieneza dini ya Allaah, wakiwafundisha watu Shari´ah Yake, wakiwawekea wazi ´Aqiydah ambayo Allaah amewatumiliza Mitume Yake. Nayo ni kumtakasia ´ibaadah Allaah Mmoja pekee na sambamba na hilo kuacha kuabudia vengine asiyekuwa Yeye katika miti, mawe, masanamu na venginevyo. Lengo asiombwe mwingine isipokuwa Allaah pekee, asitakwe uokozi mwingine asiyekuwa Yeye, kusihukumiwe isipokuwa Shari´ah Yake, kusiswaliwe kwa ajili ya mwingine isipokuwa Yeye, asiwekewe nadhiri mwingine asiyekuwa Yeye na ´ibaadah nyinginezo. Aliwabainishia watu kwamba ´ibaadah ni haki ya Allaah na akawasomea Aayah zilizopokelewa kuhusiana na hilo. Mfano wake ni maneno Yake (Subhaanah):

يَا أَيُّهَا النَّاسُ اعْبُدُوا رَبَّكُمُ

“Enyi watu! Mwabuduni Mola wenu.”[1]

وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ

“Mola wako ameamuru kwamba: “Msiabudu isipokuwa Yeye pekee.”[2]

إِيَّاكَ نَعْبُدُ وَإِيَّاكَ نَسْتَعِينُ

”Wewe Pekee tunakuabudu na Wewe Pekee tunakuomba msaada.”[3]

فَلَا تَدْعُوا مَعَ اللَّـهِ أَحَدًا

“Hivyo basi msiombe yeyote pamoja na Allaah.”[4]

قُلْ إِنَّ صَلَاتِي وَنُسُكِي وَمَحْيَايَ وَمَمَاتِي لِلَّـهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ لَا شَرِيكَ لَهُ ۖ وَبِذَٰلِكَ أُمِرْتُ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُسْلِمِينَ

“Sema: “Hakika swalah yangu, kichinjwa changu, uhai wangu na kufa kwangu ni kwa ajili ya Allaah pekee, Mola wa walimwengu, hali ya kuwa hana mshirika, na kwa hayo ndio nimeamrishwa, nami ni Muislamu wa kwanza.”[5]

Wakasubiri juu ya hayo subira kubwa na wakapambana katika njia ya Allaah mapambano makubwa – Allaah awawie radhi nao wamuie radhi.

[1] 02:21

[2] 17:23

[3] 01:05

[4] 72:18

[5] 06:162-163

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ad-Da´wah ilaa Allaah wa Akhlaaq-id-Du´aah, uk. 10-11
  • Imechapishwa: 31/05/2023