03. Kupangusa juu ya soksi za ngozi na za kawaida zilizochanika

Ama kupangusa juu ya soksi za ngozi au soksi iliyochanika, wamekhitalifiana sana katika hilo. Wengi wao wanakataza kupangusa, licha ya tofauti yao ndefu miongoni mwao, utaiona katika vitabu virefu vya Fiqh na katika ”al-Muhallaa”. Wengine wameona kwamba inajuzu, maoni ambayo ndio tunayachagua. Hoja yetu ni kwamba msingi ni kufaa. Kwa hiyo anayekataza na akaweka sharti ya kuwa salama na kuchanika au akaweka mpaka, basi hilo linarejeshwa kutokana na maneno yake Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Kila sharti lisilokuwa katika Kitabu cha Allaah basi ni batili.”[1]

Isitoshe imesihi kutoka kwa ath-Thawriy kwamba amesema:

”Paka juu yake muda wa kuwa mguu wako unashikamana nayo. Je, unafikiri kuwa soksi za Wahajiri na Wanusuraji zilikuwa vyengine kama sio kuchanika, kupasuka na zimeviringishwa viraka?”[2]

Ibn Hazm amesema:

”Ikiwa katika soksi za ngozi au kitu kingine kinachovaliwa mguuni kina tundu dogo, kubwa kwa urefu au upana, na ikaonekana sehemu ya mguu, iwe ni sehemu ndogo au kubwa au miguu yote miwili, basi yote hayo ni sawa; kupaka juu ya yote hayo kunajuzu muda wa kuwa kunabakia kitu kinachoshikamana na miguu. Haya ndio maoni ya Sufyaan ath-Thawriy, Daawuud, Abu Thawr, Ishaaq bin Raahawayh na Yaziyd bin Haaruun.”

Kisha akataja maneno ya wanazuoni wanaoikataza kwa namna zilivyo tofauti na zenye kupingana, kisha akayaraddi, na akabainisha kwamba hayo hayana dalili isipokuwa maoni tu na akamalizia hilo kwa kusema:

”Lakini haki katika hilo ni yale yaliyokuja nayo Sunnah yenye kubainisha Qur-aan kwamba hukumu ya nyayo mbili ambazo hazina kitu chochote kinachovaliwa juu yake cha kufutwa juu yake ni kuoshwa na hukumu yake ikiwa juu yake kuna kitu kinachovaliwa ni kufutwa juu ya kitu hicho. Sunnah imekuja namna hii:

وَمَا كَانَ رَبُّكَ نَسِيًّا

“Mola wako si Mwenye kusahau kabisa.”[3]

Hakika wakati Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipowaamrisha kufuta juu ya soksi za ngozi na vyenginevyo vinavyovaliwa katika miguu alijua kwamba soksi za ngozi, soksi za kawaida na vinginevyo katika vinavyovaliwa juu ya miguu vipo vilivyopasuka mpasuko mkubwa na mdogo, na visivyopasuka, na vyekundu, vyeusi kwa vyeupe, vipya kwa vilivyochakaa. Licha ya hivo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakubagua baadhi ya hivyo pasi na vyengine. Lau hukumu ya hilo katika dini ingelikuwa inatofautiana, basi Allaah (Ta´ala) asingeacha kuifafanua, wala asingepuuza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ni wajibu juu yake kubainisha. Allaah amlinde na hilo. Ikathibiti kwamba hukumu yake ni kufuta katika kila hali. Kufuta hakulazimishi kuenea kote kwa mujibu wa lugha ambayo tumezungumzishwa kwayo.”[4]

Shaykh-ul-Islam Ibn Taymiyyah amesema:

”Kwa mujibu wa moja ya maoni mawili ya madhehebu ni kwamab inajuzu kupangusa juu ya vitambaa vilivyofungwa mguuni. Maoni hayo ameyapokea Ibn Tamiym na wengineo. Hukumu hiyohiyo inatumika juu ya soksi zilizochanika muda wa kuwa zinaitwa soksi na mtu anaweza kuzitembelea. Haya ndio maoni ya zamani ya ash-Shaafi´iy, chaguo la Abul-Barakaat na wengineo miongoni mwa wanazuoni.”[5]

Maoni hayohayo ar-Raafi´iy ameyanasibisha kwa wanazuoni wengi na akajengea hoja kwamba kusema kuwa haijuzu kufuta kunabana mlango wa ruhusa, kwa hiyo ni wajibu kuzipangusa[6]. Hakika amepatia (Rahimahu Allaah)!

[1] al-Bukhaariy (2168) na Muslim (1504).

[2] ´Abdur-Razzaaq (753) na kupitia kwake al-Bayhaqiy (1/283).

[3] 19:64

[4] al-Muhallaa (2/100).

[5] al-Ikhtiyaaraat al-Fiqhiyyah, uk. 13.

[6] Sharh-ul-Wajiyz (2/370).

  • Muhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Itmaam-un-Nush fiy Ahkaam-il-Mash, uk. 84-86
  • Imechapishwa: 22/04/2026