03. Kumwacha imamu katika Tarawiyh kwa kuwa eti amezidisha juu ya Rak´ah 11

Swali 3: Mtu akiswali nyuma ya imamu anayezidisha zaidi ya Rak´ah kumi na moja aafikiane naye au aondoke zake baada ya kukamilisha Rak´ah kumi na moja?

Jibu: Sunnah ni kuafikiana na imamu. Akiondoka kabla ya imamu kumaliza hatopata ujira wa kusimama usiku mzima. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kusimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi huandikiwa ameswali usiku mzima.”[1]

Yote haya ni kwa ajili ya kutuhimiza kuchunga kubaki pamoja na imamu mpaka atakapomaliza. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliafikiana na imamu wao katika jambo linalozidi juu ya kile kilichowekwa katika Shari´ah katika swalah moja. Hayo yalitokea pamoja na kiongozi wa waumini ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) wakati aliposwali kikamilifu Minaa katika hajj. Aliswali Rak´ah nne licha ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan mwenyewe mwanzoni mwa uongozi wake, mpaka kulipopita miaka minane, walikuwa wakiswali Rak´ah mbilimbili. Kisha baadaye akaswali Rak´ah nne. Maswahabah walimkemea jambo hilo. Pamoja na hivyo walikuwa wakimfuata na wakiswali pamoja naye Rak´ah nne. Basi ikiwa huu ndio mwongozo wa Maswhabah, nayo ni ile pupa ya kumfuata imamu, wana nini baadhi ya watu pindi wanapomuona imamu anazidisha juu ya ile idadi ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi juu yake ambayo ni Rak´ah kumi na moja, basi  wanaondoka na kumwacha katikati ya swalah. Haya tunayashuhudia baadhi ya watu katika msikiti Mtakatifu wanaondoka kabla ya imamu kumaliza kwa hoja eti imamu amezidisha juu ya kile kilichosuniwa ambacho ni Rak´ah kumi na moja.

[1] Abu Daawuud (1375) na at-Tirmidhiy (806). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 11-12
  • Imechapishwa: 10/04/2021