Swali: Kitendo cha Jibriyl kumfunza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) Qur-aan ndani ya Ramadhaan tunaweza kuchuma faida ya fadhilah za kukhitimisha Qur-aan?

Jibu: Tunachuma faida ya kufundishana na kwamba inapendeza kwa muumini kumfunza Qur-aan yule ambaye inamfaidisha na kumnufaisha. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsomea Jibriyl ili aweze kufaidika. Jibriyl ndiye anayetoka kwa Allaah (´Azza wa Jall). Yeye ndiye balozi kati ya Allaah na Mitume. Ni lazima Jibriyl amfaidishe Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) mambo kutoka kwa Allaah kwa njia ya kusimamisha herufi za Qur-aan na maana ya yale aliyokusudia Allaah. Kwa hivyo mtu akijifunza kutoka kwa ambaye atamsaidia kuifahamu Qur-aan na mwenye kumsaidia kutamka vizuri matamshi yake, ni jambo linalotakikana. Ni kama ambavo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimsomea Jibriyl. Haina maana kwamba Jibriyl ni mbora zaidi kuliko Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Lakini hata hivyo Jibriyl ni mjumbe anayetoka kwa Allaah ambaye anamfikishia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yale ambayo Allaah amemwamrisha upande wa Qur-aan yenyewe, matamshi yake na maana yake. Kwa hiyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anafaidika kutoka kwa Jibriyl kutokana na kipengele hiki. Haina maana kuwa Jibriyl ni mbora kuliko yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Bali yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ndiye kiumbe bora na ndiye mbora kuliko Malaika. Lakini kufundishana ilikuwa ni jambo lina kheri kubwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na juu ya ummah. Ni masomo yenye kutoka kwa Allaah na ili aweze kufaidika na yale yenye kutoka kwa Allaah.

Kuna faida nyingine ambayo kufundishana usiku ni bora kuliko mchana. Kufundishana huku ilikuwa wakati wa usiku. Inatambulika kuwa usiku inakuwa ni karibu zaidi kwa moyo kukusanyika, kuhudhuria kwake na kufaidika zaidi kuliko mtu anavyofaidika mchana.

Faida nyingine ni ule usuniwaji wa kusomeshana na kwamba ni kitendo chema hata kama si ndani ya Ramadhaan. Ni jambo lina faida kwa wote wawili. Wakiwa zaidi ya watu wawili ni sawa wakafaidishana kila mmoja kutoka kwa ndugu yake na wakatiana moyo juu ya kusoma. Pengine mtu asipate uchangamfu pindi anapoketi peke yake. Lakini anapokuwa na mwanafunzi au wanafunzi wake wanasomeshana, basi kunamtia moyo na uchangamfu zaidi. Ukiongezea ile faida inayopatikana kati yao katika kukumbushana na kusomeana mambo ambayo pengine yakawa ni magumu kwao. Yote hayo yana kheri kubwa.

Isitoshe kingine kinachoweza kufahamika kutokana na hilo ni kwamba imamu kuwasomea waswaliji Qur-aan yote ndani ya Ramadhaan ni aina fulani ya kusomeshana huku. Kwa sababu kufanya hivo anawafaidisha na Qur-aan yote. Kwa ajili hiyo imamu Ahmad (Rahimahu Allaah) alikuwa anapenda wale wanaowaongoza katika swalah wawakhitimishie Qur-aan. Kitendo hicho ni aina fulani ya Salaf katika kupenda kusikiliza kwao Qur-aan yote. Hata hivyo hii hailazimu mtu afanye haraka na asifanye utulivu katika kisomo chake na asichunge unyenyekevu na utulivu. Bali kuyachunga mambo haya ni muhimu zaidi kuliko kuchunga kukhitimisha.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Min A´maal Ramadhwaan, uk. 06-07
  • Imechapishwa: 31/03/2023