03. Kuchelewesha Fajr mpaka kupambazuke alfajiri ya kweli

Swali 03: Baadhi wanachelewesha swalah ya Fajr mpaka kupambazuke alfajiri ya kweli (الإسفار) kwa kujengea hoja kwamba kumepokelewa Hadiyth inayosema:

“Ichelewesheni Fajr. Kwani kufanyo hivo kuna ujira mkubwa zaidi.”

Je, Hadiyth hii ni Swahiyh? Ni vipi itaoanishwa na Hadiyth inayosema:

“Swalah ndani ya wakati wake”?

Jibu: Hadiyth uliyotaja ni Swahiyh. Imepokelewa na Imaam Ahmad na watunzi wa Sunan kwa cheni ya wapokezi Swahiyh kupitia kwa Raafiy´ bin Khadiyj (Radhiyj Allaahu ´anh). Haipingani na Hadiyth Swahiyh zinazofahamisha kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Subh katika giza la mwisho wa usiku linapochanganyikana na mwanga wa asubuhi. Vilevile haipingani na Hadiyth inayosema:

“Swalah ndani ya wakati wake.”

Hakika si venginevyo maana yake kwa mujibu wa maoni ya kikosi cha wanazuoni wengi ni kuchelewesha swalah ya Fajr mpaka pale kutapobainika alfajiri. Kisha inaswaliwa kabla ya kupotea lile giza la mwisho wa usiku linalochanganyikana na mwanga wa asubuhi. Hivo ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifanya. Isipokuwa tu katika Muzdalifah. Bora ni kuiswali mapema punde tu baada ya alfajiri kupambazuka. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya hivo katika hajj ya kuaga. Namna hiyo ndivo zinaoanishwa Hadiyth zilizothibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu wakati wa swalah ya Fajr. Yote hayo ni kwa njia ya ule ubora.

Vilevile inafaa kuichelewesha Fajr mpaka mwishoni mwa wakati kabla ya jua kuchomoza. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wakati wa Fajr ni kuanzia pale inapochomoza alfajiri muda wa kuwa jua halijachomoza.”

Ameipokea Imaam Muslim katika “as-Swahiyh” yake kupitia kwa ´Abdullaah bin ´Amr bin al-´Aasw (Radhiya Allaahu ´anhumaa).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Muhimmah, uk. 04-05
  • Imechapishwa: 08/08/2022