Haafidhw Ibn Hajar al-´Asqalaaniy (Rahimahu Allaah) amesema:

675- Mama wa waumini Hafswah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyelala na nia kabla ya alfajiri hana swawm.”[1]

Wameipokea watano. an-Nasaa´iy na at-Tirmidhiy wameegemea zaidi kwamba maneno hayo ni ya Swahabah. Ibn Khuzaymah na Ibn Hibbaan wamesahihisha Hadiyth kuwa ni maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Katika upokezi wa ad-Daaraqutwniy imekuja:

“Hana swawm yule ambaye hakulala na swawm usiku.”[2]

676- ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema:

“Siku moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliingia kwangu akasema: “Mna chochote?” Nikasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Basi mimi nimefunga.” Akaja siku nyingine kwangu nikasema: “Nimepata tende ya kusagwasagwa.” Akasema: “Nionyeshe nayo. Nilikuwa nimefunga.” Baadaye akaila.”[3]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hadiyth hizi zinafahamisha kwamba mtu akitaka kufunga basi ni lazima aweke nia kabla ya alfajiri. Hii inahusiana na swawm ya faradhi. Kuhusu swawm ya sunnah anaweza kunuia wakati wa mchana ikiwa hakula au kunywa. Lakini inaweza kuwa tatizo kwa mtu ikiwa ni usiku wa tarehe 30 Sha´baan na khabari hazijatoka kabla hajalala. Je, katika hali hii inafaa akalala na nia kwamba ikiwa kesho ni Ramadhaan basi mimi nitakuwa mwenye kufunga? Ndio, inafaa. Ikibainika kuwa ni Ramadhaan, basi swawm yako ni sahihi.

Kuhusu funga ya sunnah, hakuna neno mtu akanuia wakati wa mchana ikiwa mtu hajala, hajanywa na wala hajafanya chochote kinachofunguza. Dalili ya hilo ni:

“Mna chochote?” Nikasema: “Hapana.” Ndipo akasema: “Basi mimi nimefunga.”

Bi maana kuanza hivi sasa mimi nimefunga.

[1] Ahmad (6/287), Abu Daawuud (2454), at-Tirmidhiy (730), an-Nasaa’iy (2331), Ibn Maajah (1700) na Ibn Khuzaymah (1933).

[2] ad-Daaraqutwniy (2214).

[3] Muslim (1154).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ash-Sharh al-Mukhtaswar ´alaa Buluugh-il-Maraam (2/407-409)
  • Imechapishwa: 23/04/2020