02. Ulazima wa viumbe wote kuingia katika Uislamu

Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Na yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kutoka kwake, naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

إِنَّ الدِّينَ عِندَ اللَّـهِ الْإِسْلَامُ

 “Hakika dini mbele ya Allaah ni Uislamu.” (03:19)

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate vichochoro [vinginevyo]; vikakufarikisheni na njia Yake!” (06:153)

Mujaahid amesema:

“Vichochoro ni Bid´ah na utata.”

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesema kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuzusha katika amri yetu hii yasiyokuwemo yatarudishwa.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yule mwenye kufanya tendo lisiloafikiana na amri yetu litarudishwa.”[2]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ummah wangu wote utaingia Peponi isipokuwa yule asiyetaka.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Ni nani atayekataa?” Akasema: “Yule mwenye kunitii, ataingia Peponi, na yule mwenye kuniasi amekataa.”[3]

al-Bukhaariy amepokea kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Watu wanaochukiwa zaidi na Allaah ni watatu; mtenda dhambi Haram, mwenye kutaka katika Uislamu mwenendo wa kipindi cha kikafiri na mwenye kuomba damu ya mtu muislamu pasi na haki ili amwage damu yake.”[4]

MAELEZO

Mwenye kutaka katika Uislamu mwenendo wa kipindi cha kikafiri – Lililo la lazima kwa mja ni yeye kushikamana barabara na Uislamu na atahadhari kutokamana na mienendo ya kipindi cha kikafiri. Kutenda kwa mujibu wa Uislamu, japo ni kwa uchache, ndio jambo linalonufaisha. Ama kufanya bidii kwa mujubu usiokuwa wa Uislamu na Sunnah kunamdhuru mtu na wala hakunufaishi. Ni lazima kwa viumbe wote kushikamana barabara na Uislamu, kujifungamanisha na dini ya Allaah na kuufuata katika kila jambo. Mtu afanye yote hayo hali ya kumtakasia nia Allaah na kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[2] Muslim (1718).

[3] al-Bukhaariy (7280).

[4] al-Bukhaariy (6882).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Fadhwl-il-Islaam, uk. 08-09
  • Imechapishwa: 08/10/2020