02. Tofauti ya muumini na asiyekuwa muumini katika kukabiliana na mitihani mbalimbali

Mwengine anayapokea yale mazito yaliyomfika kwa shari, jeuri na kuchupa mpaka. Matokeo yake tabia yake inapondoka. Anayapokea kama wanavyoyapokea wanyama kwa pupa na kukata tamaa. Ukiongezea kwamba moyo wake unakuwa si wenye kutulizana. Bali anakuwa ni mwenye kuzongwa kwa njia mbalimbali; amesononeka kwa njia ya kuondoka vile vitu anavopenda, wingi wa vile vitu ambavo mara nyingi hujitokeza katika jambo hilo, kwa njia ya kwamba nafsi hazisimami katika jambo moja bali zinakuwa ni zenye shauku katika mambo mengine ambavo huenda zikavipata na huenda zisivipate. Hata kama tutakadiria kwamba mtu atavipata lakini atasononeka katika ile njia nyingine iliyotajwa. Anakuwa ni mwenye kuyapokea yale mambo yenye kuchukiza kwa kusikitika, kuvunjika moyo, kuwa na khofu na kuongea yasiyofaa. Usiulize yale maisha mabaya yatayomtokea, ugonjwa wa kufikiria, wa viungo na ile khofu ambayo inaweza kumfikisha katika hali ambayo ni mbaya na yenye mfazaiko zaidi. Kwa sababu hatumai thawabu wala subira yenye kumliwaza na kumfanyia wepesi.

Yote haya ni yenye kushuhudiwa kwa uzoefu. Mfano mmoja wa sampuli hizi pale ambapo utauzingatia na kuuteremsha juu ya hali za watu, basi utaona tofauti kubwa kati ya muumini anayeitendea kazi imani yake na ambaye hayuko hivo. Hayo si vyenginevo ni kwa sababu dini inakokoteza mtu kukinaika na riziki ya Allaah na katika yale aliyowatunuku waja katika fadhilah na karama mbalimbali.

Muumini anapopewa mtihani kwa maradhi, ufakiri au mfano wake katika vitu ambavo mtu yeyote vinaweza kumtokezea, basi utamuona ni mwenye kutulizana jicho lake kutokana na imani yake, kule kukinaika alikonako na kuridhia kile Allaah alichomgawia. Hutumuona ni mwenye kutafuta jambo ambalo Allaah hakumkadiria. Humtazama ambaye yuko chini yake na wala hamtazami ambaye yuko juu yake. Si ajabu ukaona tabasamu, furaha na raha yake ikashinda ya yule ambaye anapata furaha zote za kidunia endapo mtu huyo hajapewa kukinai. Ni kama ambavo utamuona huyu ambaye hatendi kwa mujibu wa imani yake, pale anapopewa sehemu ya ufakiri au akakosa baadhi ya starehe za kidunia, basi utamuona katika huzuni na misononeko ya hali ya juu.

Mfano mwingine ni kwamba kukijitokeza sababu za khofu na mtu akafikwa na mambo ya kumyumbisha, basi utamuona mtu mwenye imani ya kweli moyo wake uko imara, nafsi yake imetulizana, yuko makini katika kuipeleka na kuyafanya mepesi kutokana na jambo hili lililombabaisha kwa yale maneno na matendo yaliyo ndani ya uwezo wake. Unamuona kuwa ameituliza nafsi yake kwa jambo hili zito lililompata. Mambo kama haya yanamstarehesha mtu na kukithibitisha kifua chake.

Upande mwingine utamuona yule asiyekuwa na imani yuko kinyume na hali hii. Pindi kunapotokea mambo yenye kukhofisha, basi moyo wake unakuwa wenye kuogopa, mwili wake unabadilika, fikira zake zinasambaratishwa na anaingiwa na khofu, woga na pia anakusanyikiwa na khofu ya nje na wasiwasi wa ndani ambao hauwezi kuelezwa. Watu aina hii wasipopata baadhi ya zile sababu za kawaida ambazo zinahitajia mtu ajipe mazoezi mengi, basi nguvu yao huporomoka na viungo vyao hukaza. Hayo ni kwa sababu ya kukosa imani inayomsukuma katika subira na khaswakhaswa katika hali nzitonzito kama za kusononesha na za kutisha.

Mwema, mwovu, muumini na kafiri wote wanashirikiana katika kule kuuchuma ushujaa na pia tabia za kimaumbile zinazodogesha yale mambo yanayotia khofu na kuyalainisha. Lakini hata hivyo muumini anapambanuka kwa nguvu ya imani, subira yake, kumtegemea kwake Allaah na kutarajia thawabu Zake, mambo yanayozidisha ule ujasiri wake na kuwepesisha ule ukubwa wa khofu na majanga. Amesema (Ta´ala):

إِن تَكُونُوا تَأْلَمُونَ فَإِنَّهُمْ يَأْلَمُونَ كَمَا تَأْلَمُونَ ۖ وَتَرْجُونَ مِنَ اللَّـهِ مَا لَا يَرْجُونَ

“Mkiwa mnaumia, basi nao pia wanaumia kama mnavyoumia na mnataraji kutoka kwa Allaah yale wasiyoyataraji wao.”[1]

Isitoshe pia wanapata msaada wa Allaah na upamoja Wake maalum mambo yanayoondosha zile khofu. Amesema (Ta´ala):

وَاصْبِرُوا ۚ إِنَّ اللَّـهَ مَعَ الصَّابِرِينَ

“Subirini! Hakika Allaah yupamoja na wenye kusubiri.”[2]

[1] 04:104

[2] 08:46

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 08/06/2020