Je, talaka inakuwa mkononi mwa mwanamke au mwanaume? Kimsingi ni kwamba talaka inakuwa mkononi mwa mwanamme kwa mujibu wa dalili ya Qur-aan na Sunnah. Amesema (Ta´ala):

لَّا جُنَاحَ عَلَيْكُمْ إِن طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ مَا لَمْ تَمَسُّوهُنَّ أَوْ تَفْرِضُوا لَهُنَّ فَرِيضَةً

”Hapana dhambi kwenu mkiwataliki wanawake ambao hamkuwagusa au kuwawekea wazi mahari yao.”[1]

وَإِنْ أَرَدتُّمُ اسْتِبْدَالَ زَوْجٍ مَّكَانَ زَوْجٍ وَآتَيْتُمْ إِحْدَاهُنَّ قِنطَارًا

“Mkitaka kubadlisha mke mahali pa mke na mkampa mmoja wao [zawadi ya] mirundi ya mali.”[2]

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نَكَحْتُمُ الْمُؤْمِنَاتِ ثُمَّ طَلَّقْتُمُو

“Enyi walioamini! Mnapofunga ndoa na waumini wa kike kisha mkawataliki… ”[3]

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ

“Ee Nabii!  Mtakapowataliki wanawake, basi watalikini katika wakati wa twahara zao.”[4]

Imekuja katika Hadiyth kupitia kwa Ibn ´Umar ambaye amesema:

”Nilimuoa mwanamke niliyempenda na baba yangu alikuwa akimchukia. Ndipo baba yangu akaniamrisha kumtaliki ambapo nikakataa. Baadaye nikamtajia hilo Mtume ambaye alisema: ”Ee ´Abdullaah mwana wa ´Umar, mwache mwanamke wako!”[5]

Ameipokea at-Tirmidhiy ambaye amesema kuwa Hadiyth ni nzuri na Swahiyh. Ameipokea al-Haakim pia naye pia akaisahihisha.

Imepokelewa kutoka kwa Ibn ´Umar pia kwamba alimtaliki mke wake hali ya kuwa na hedhi. ´Umar akamweleza hilo Mtume ambapo akasema:

”Mwamrishe amrejee, kisha amtaliki akiwa amesafika au mjamzito.”[6]

Ameipokea Ibn Maajah (2023).

Mwanamke wa Qays bin Shammaas ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia:

”Kubali shamba kisha umtaliki.”[7]

Tutataja maana ya Hadiyth katika masuala mengine kwa ukamilifu wake.

[1] 02:236

[2] 04:20

[3] 33:49

[4] 65:01

[5] at-Tirmidhiy (04/169) (7653), al-Haakim katika ”al-Mustadrak” (7653). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah (2088).

[6] Ibn Maajah (2023). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Swahiyh Ibn Maajah (1643).

[7] al-Bukhaariy (5673).

  • Mhusika: Shaykh Jamaal bin Furahyaan al-Haarithiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Twalaaq – asbaabuhu wa ´ilaajuh, uk. 16-17
  • Imechapishwa: 26/03/2024