Shaykh-ul-Islaam Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab (Rahimahu Allaah) amesema:

Sharti ya kwanza ni Uislamu na kinyume chake ni ukafiri. Matendo ya kafiri ni yenye kurudishwa, bila ya kuzingatia sawa akifanya ´amali yoyote ile. Dalili ni Kauli Yake (Ta´ala):

مَا كَانَ لِلْمُشْرِكِينَ أَن يَعْمُرُواْ مَسَاجِدَ الله شَاهِدِينَ عَلَى أَنفُسِهِمْ بِالْكُفْرِ أُوْلَئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ وَفِي النَّارِ هُمْ خَالِدُونَ

“Si haki kwa washirikina kuamirisha misikiti ya Allaah hali ya kuwa wanajishuhudia nafsi zao kwa ukafiri. Hao yamebatilika matendo yao na katika Moto wao ni wenye kudumu.”[1]

وَقَدِمْنَا إِلَى مَا عَمِلُوا مِنْ عَمَلٍ فَجَعَلْنَاهُ هَبَاء مَّنثُورًا

”Na Tutayaendea yale waliyoyatenda ya matendo yoyote yale na Tutayafanya kuwa ni mavumbi yaliyotawanyika.”[2]

MAELEZO

Kila kitendo cha kujikurubisha kwa Allaah katika ummah huu hakimfai mwenye nacho isipokuwa ikiwa kimetanguliwa na kushuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah na kiwe kimejengwa juu ya hayo mawili. Kwa hivyo ni lazima kumtakasia matendo Allaah, nayo ndio matokeo ya ”Kushuhudia ya kwamba hapana mungu isipokuwa Allaah”. Aidha ni lazima kumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), nayo ndio matokeo ya ”Kushuhudia ya kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Kila kitendo anachofanya kafiri hakimsaidii kitu mbele ya Allaah (´Azza wa Jall), kwa sababu ya kukosa sharti ya Uislamu. Shaykh (Rahimahu Allaah) ametolea dalili ya kurudishwa nyuma matendo ya makafiri na kutokukubaliwa kwa hizo Aayah mbili katika Suurah ”at-Tawbah” na Suurah ”al-Furqaan”. Aayah ya ”at-Tawbah” imemalizika kwa kubainisha kuporomoka matendo ya makafiri. Aayah ya ”al-Furqaan” imebainisha ya kwamba matendo yao hayazingatiwi na kwamba ni kama vumbi lililotawanyika, kwa maana ya kwamba yamebatilika na kupotea bure.

[1] 09:17

[2] 25:23

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Shuruwt-is-Swalaah, uk. 5
  • Imechapishwa: 30/04/2026