Mu´aawiyah bin al-Hakam as-Sulamiy (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia:

“Nilikuwa na kondoo kati ya Uhud na Jawaaniyyah wanaochungwa na kijakazi wangu[1]. Siku moja akaja mbwa mwitu na akamchukua kondoo kutoka kwake. Mimi ni mwanaadamu wa kawaida ambaye hukasirika kama wanavyokasirika watu wengine. Nikaunyanyua mkono wangu na kumpiga kofi. Nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kumweleza yaliyopitika. Nikasikitika sana na kumwambia: “Ee Mtume wa Allaah! Si nimwache huru?” Akasema: “Mwite.” Nikamwita. Ndipo Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Allaah yuko wapi?” Akajibu: “Juu ya mbingu.” Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[2]

Ameipokea Muslim katika ”as-Swahiyh” yake.

Muhammad bin ´Amr ameeleza kutoka kwa Abu Salamah, kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh), ambaye amesimulia:

”Muhammad bin ash-Shariyd alikuja na mjakazi mweusi kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kuema: “Ee Mtume wa Allaah! Hakika mama yangu ameweka nadhiri ya kuacha huru mtumwa muumini. Ee Mtume wa Allaah, je inasihi nimuache huru huyu?” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia yule kijakazi: ”Yuko wapi Mola wako?” Akainua kichwa chake akasema: ”Juu mbinguni.” Akamuuliza: “Mimi ni nani?” Akasema: ”Wewe ni Mtume wa Allaah. Akasema: “Mwache huru, hakika yeye ni muumini.”[3]

Ameipokea Ibn Khuzaymah katika ”Kitabu-ut-Tawhiyd. Hadiyth ya kuhusu mjakazi imepokelewa kwa njia nyingi.

Abu Raziyn (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Ee Mtume wa Allaah! Ni wapi alikuwa Mola wetu kabla hajaumba viumbe Vyake?” Akasema: ”Alikuwa juu ya anga. Chini yake palikuwa hewa na juu yake palikuwa hewa. Kisha akaumba ´Arshi Yake kisha akalingana juu yake.”[4]

Ameipokea Ahmad, at-Tirmidhiy, ambaye amesahihisha Hadiyth kwa cheni yake, na Ibn Maajah.

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Wanapishana kwenu Malaika wa usiku na Malaika wa mchana. Wanakusanyika katika swalah ya Fajr na swalah ya ´Aswr. Halafu hupanda wale waliolala kwenu ambapo Mola wenu Anawauliza – ilihali ni mjuzi zaidi kuliko wao: “Mmewaachaje waja Wangu?” Wanasema: “Tumewaacha na huku wanaswali na tumewaendea na huku wanaswali.”[5]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Wahurumieni waliyoko ardhini atakuhurumieni aliyeko juu ya mbingu.”[6]

Ameisahihisha at-Tirmidhiy. Imepokelewa kwa njia zaidi ya moja.

[1] Kuna andiko lingine linalomweleza kwamba alikuwa kijakazi mweusi, ambalo amelipokea ad-Daarimiy katika ”ar-Radd ´alaa al-Mariysiy”, uk. 95, kwa cheni ya wapokezi Swahiyh.

[2] Muslim (538).

[3] Ahmad (7893), Abu Daawuud (3283) na Ibn Khuzaymah katika ”at-Tawhiyd” (81-82). Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa Ahmad Shaakir na ni nzuri na Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan Abiy Daawuud” (3283).

[4] Ahmad (4/11-12), at-Tirmidhiy (3109), aliyesema kuwa ni nzuri, na Ibn Maajah (182). Swahiyh kwa mujibu wa at-Twabariy katika ”Taariykh-ur-Rusul wal-Muluuk” (1/40), Ibn Hibbaan katika ”as-Swahiyh” (6141), Ibn-ul-´Arabiy katika ”´Aaridhwat-ul-Ahwadhwiy” (6/208) na Ibn-ul-Qayyim katika ”I´laam-ul-Muwaqqi´iyn” (4/224), nzuri kwa mujibu wa at-Tirmidhiy katika ”al-Jaamiy´” (3109) na adh-Dhahabiy katika ”al-´Uluww” (18) na ni dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Dhwa´iyf Sunan Ibn Maajah” (181).

[5] al-Bukhaariy (7429) na Muslim (632).

[6] Ahmad (2/160), Abu Daawuud (4941), at-Tirmidhiy (1924), ambaye amesema kuwa ni nzuri na Swahiyh, na al-Haakim (4/159), ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (1924).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Ahmad bin ´Abdil-Haadiy al-Maqdisiy (afk. 744)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Kalaam ´alaa Mas-alat-il-Istiwaa’ ´alaal-´Arsh, uk. 27-30§
  • Imechapishwa: 18/12/2025