02. Kunywa pombe kunaondosha imani

Tambua kwamba unywaji pombe unapelekea katika maharibifu katika dini na adhabu huko Aakhirah. Kuhusu maharibifu katika dini ni mengi ikiwa ni pamoja na:

1- Kunywa pombe ni kuondoshwa kwa imani

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hanywi pombe pindi anapokunywa hali ya kuwa ni muumini.”[1]

Yamekwishatangulia maneno ya ´Uthmaan aliyesema:

“Imani na kudumu kunywa pombe hakukusanyiki kamwe kwenye kifua cha mtu. Kimoja kinakaribia kukiondosha kingine.”

Neno “kufuru” na shirki” limetumika juu ya unywaji pombe na mnywaji pombe amefananishwa na mwabudia sanamu. ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kunywa pombe ikaingia tumboni mwake basi hazitokubaliwa swalah zake kwa saba. Akifa ndani yake basi amekufa akiwa ni kafiri. Endapo ataondokwa na fahamu zake ambapo akapitwa na chochote miongoni mwa mambo ya faradhi, basi swalah zake hazitokubaliwa kwa muda wa siku arobaini. Akifa ndani yake basi amekufa akiwa ni kafiri.”[2]

Upokezi huu umepokelewa kupitia njia nyingi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kutoka kwa ´Abdullaah. Lakini hata hivyo yanaonekana ni kama vile ni maneno ya Swahabah.

Khaythamah ameeleza kwamba ´Abdullaah amesema:

“Unywaji pombe ndio dhambi kubwa kabisa. Yule mwenye kuinywa mchana basi anashinda akiwa ni mshirikina, na yule mwenye kuinywa usiku basi analala akiwa ni mshirikina.”[3]

Ibn ´Abbaas amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Chapombe akifa basi atakutana na Allaah kama vile mwabudia sanamu.”[4]

Ibn-ul-Jawziy ameitaja Hadiyth hiyo:

“Mnywaji pombe ni kama mtu ambaye anamwabudu al-Laat na al-´Uzzaa.”[5]

Hilo ni kwa sababu chapombe huishikilia na anakaribia kupumzika nayo, hivyo anakuwa kama mshirikina anavoshikilia sanamu lake. Ni kama alivosema ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) juu ya mchezo wa Sataranji. Imepokelewa kutoka kwake ya kwamba amesema:

“Waabudia moto walikuwa na dini na walikuwa na mfalme aliyekuwa akinywa pombe. Siku moja akalewa na hivyo akamwingilia dada yake. Halafu akadai kuwa Allaah ameihalalisha. Kila ambaye alisema kinyume na hivo wakatupwa ndani ya mashimo ya moto. Mwanamke mmoja akaletwa akiwa amemkumbatia mwanae. Mtoto yule akasema: “Ee mama! Wacha utupwe. Hakika adhabu ya dunia ni nyepesi ukilinganisha na adhabu ya Aakhirah.”

Ameipokea Ya´quub bin Shaybah.

Kila ambavo mtu atadumu kunywa pombe na akaishikilia, ndivo imani yake itashuka chini, kudhoofika na kumwondoka zaidi. Kuna khatari imani kumwondoka kabisa wakati wa kifo, hayo yametokea katika masimulizi yaliyotajwa na ´Abdul-´Aziyz bin Abiy Rawwaad. ´Abdul-´Aziyz alikuwa akisema:

“Yaogopeni madhambi. Kwani hakika ndio yaliyomwangusha.”[6]

´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Afueni kuzini na kuiba kuliko kunywa pombe. Kwa sababu inafikia kipindi ambapo mlevi hamtambui Mola wake.”[7]

Kuna upokezi kama huo uliopokelewa wa kiisraaiyl[8].

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kila chenye kulevya na kuzuia swalah[9]. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللَّـهِ وَعَنِ الصَّلَاةِ ۖ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ

“Hakika si vyenginevyo shaytwaan anataka kutia kati yenu uadui na bughudha katika pombe na kamari na akuzuieni kutokamana na kumdhukuru Allaah na swalah, hivyo basi, je, mtakoma?”[10]

Mja hawi mwenye kufikia furaha na mafanikio pasi na kumtaja Allaah na swalah. Kwa ajili hiyo ndio maana kukatazwa kila kinachomzuia mtu kutokamana na jambo hilo.

[1] al-Bukhaariy (2475) na Muslim (57).

[2] an-Nasaa’iy (5179).

[3] Ibn Abiy Shaybah katika ”al-Muswannaf” (24087).

[4] Ahmad (1/272) na Ibn Hibbaan (5347).

[5] al-´Ilal al-Mutanaahiyah (2/670). Ibn-ul-Djawziy amesema:

”Hadiyth hii haikusihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).”

[6] Ibn Abiyd-Dunyaa katika ”Kitaab-ul-Muhtadhariyn”, uk, 203-204

[7] Ibn Abiyd-Dunyaa katika ”Dhamm-ul-Muskir”, uk. 52

[8] Shu´ayb bin Harb amesema:

”Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema: ”Mja Wangu kuua kunapendeza zaidi kwangu kuliko kunywa pombe. Kwa sababu pindi anapokuwa amelewa hanitambui.” (Ibn Abiyd-Dunyaa katika ”Dhamm-ul-Muskir”, uk. 52)

[9] Muslim (1733).

[10] 5:91

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 9-12
  • Imechapishwa: 20/07/2020