01. Pombe – funguo ya shari zote

ad-Daaraqutwniy amepokea kwa cheni ya wapokezi dhaifu kupitia kwa Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anh) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

”Pombe ndio mama ya machafu yote. Yule mwenye kuinywa atamwingilia mama yake, shangazi yake na mama yake mdogo.”[1]

´Uthmaan (Radhiya Allaahu ´anh) pia amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ingawa sahihi ni kwamba ni maneno yake mwenyewe:

“Jiepusheni na pombe, kwani ndio msingi wa machafu yote. Kuna bwana mmoja ambaye alikuwa kabla yenu alikuwa mfanya ´ibaadah na akijiepusha na watu. Sambamba na hilo kuna mwanamke mmoja mpotevu alikuwa amefungamana naye. Mwanamke yule akamwagizia mfanyikazi wake aliyesema: “Anakwita kwa ajili ya ushahidi.” Akaingia ndani. Kila alipopita kwenye mlango basi mwanamke yule anaufunga. Mpaka mwanamme yule alipofika kwa mwanamke mmoja mrembo. Kwa mwanamke huyo kulikuweko kijana na chombo cha pombe. Mwanamke yule akasema: “Nimekuita ili umuue kijana huyu au ulale na mimi au upige glasi moja.” Ukikataa basi nitapiga makelele na kukufedhehesha.” Alipoona kuwa hana njia nyingine isipokuwa kufanya jambo akamwambia mwanamke yule: “Nimiminie glasi moja.” Akamiminiwa glasi moja.” Kisha akasema: “Nizidishie.” Mwishowe akamwingilia na akamuue kijana yule. Hivyo jiepusheni na pombe. Kwani hakika imani na kudumu kunywa pombe hakukusanyiki kamwe kwenye kifua cha mtu. Kimoja kinakaribia kukiondosha kingine.”[2]

ad-Daaraqutwniy amepokea tena kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliyesema:

“Pombe ndio mama ya machafu yote.”[3]

Imepokelewa kutoka kwake pia kwamba amesema:

“Nimeyasoma katika Tawraat.”[4]

Katika “al-Musnad” ya Ibn Wahb imetajwa kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ndio dhambi kubwa na ndio msingi wa machafu. Hivyo msinywe pombe. Kwani ndio funguo ya shari zote. Yule mwenye kuinywa ataacha swalah, atamwingilia mama yake, shangazi yake na mama yake mdogo.”

Mu´aadh (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Msinywe pombe. Kwani hakika ndio kichwa cha machafu yote.”[5]

´Uthmaan amesema:

“Pombe ndio mkusanyiko wa machafu yote.”

´Uthmaan amesema tena:

“Nakutahadharisheni na pombe. Kwani hakika ndio funguo ya shari zote. Kuna bwana mmoja aliletwa na akaambia: “Ima uchanechane kitabu hiki, umuue mtoto huyu, usujudie msalaba huu, ufanye machafu na mwanamke huyu au unywe glasi hii.” Hakuona jambo jepesi kama kunywa glasli ile na hivyo akanywa glasi, akafanya machafu na mwanamke, akamuua mtoto yule, akachanachana kitabu na akasujudia msalaba. Ndio funguo ya shari zote.”[6]

Mujaahid amesema:

“Ibliys anasema: “Pindi mwanadamu anapolewa basi hushika kwenye pete yake ya pua na tukamwelekeza kule tunakotaka.”[7]

Wahb bin Munabbih amesema:

“Shaytwaan anasema: “Pindi anapolewa mwanadamu basi tunamwelekeza katika matamanivu yote kama anavyoongozwa ngamia kwenye sikio lake.”[8]

Ibn Abiyd-Dunyaa amesimulia bwana aliyeota namna mahujaji wote ´Arafah walisamehewa isipokuwa mtu mmoja. Wakati ndoto hiyo ilipopelekwa kwa bwana yule akamuuliza sababu iliofanya hivo ambapo akajibu kuwa alikuja hali ya kuwa amelewa na mama yake akamkataza ambapo bwana huyo akamchukua na kumtupa kwenye oveni iliokuwa inawaka moto[9]. Hata Ibn-ul-Jawziy ameitaja ndoto hiyo kwa urefu zaidi na njia ya kigeni.

Ibn Marduuyah ameeleza kutoka kwa ´Abdullaah bin ´Amr aliyesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliwasimulia kuhusu mfalme wa wana wa israaiyl aliyemkamata bwana mmoja na akampa chaguo kati ya kunywa pombe, kumuua mtu, kuzini, kula nyama ya nguruwe au kuuliwa.” Akachagua kunywa pombe. Alipokunywa pombe hiyo akafanya yale mambo yote aliyokhiyarishwa.”[10]

Kisa cha Haaruut na Maaruut kina maana kama hii. Kimetolewa na Ahmad kupitia kwa Ibn ´Umar kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo cheni ya wapokezi imetiwa dosari. Imesemekana vilevile kwamba kimesimuliwa kutoka kwa Ka´b.[11]

[1] ad-Daaraqutwniy (4/247) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Kabiyr” (1/164).

[2] an-Nasaa’iy (5666).

[3] ad-Daaraqutwniy (4/247).

[4] al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (10/222).

[5] Ahmad (5/238).

[6] al-Bayhaqiy katika ”as-Sunan al-Kubraa” (8/288).

[7] Ibn Abiy Dunyaa katika ”Dhamm-ul-Muskir”, uk. 67

[8] Abu Nu´aym katika ”Hilyat-ul-Awliyaa’” (4/52-53).

[9] Ibn Abiy Dunyaa katika ”Dhamm-ul-Muskir”, uk. 76

[10] al-Haakim (7236) na at-Twabaraaniy katika ”al-Mu´jam al-Awsatw” (363).

[11] Ahmad (2/134).

  • Mhusika: Imaam Zayn-ud-Diyn bin Rajab al-Hanbaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Dhamm-ul-Khamr, uk. 5-9
  • Imechapishwa: 20/07/2020