02. Imamu anayezidisha Rak´ah kumi na moja

Swali: Mtu akiswali nyuma ya imamu anayezidisha zaidi ya Rak´ah kumi na moja aafikiane naye au aondoke zake baada ya kukamilisha Rak´ah kumi na moja?

Jibu: Sunnah ni kuafikiana na imamu. Akiondoka kabla ya imamu kumaliza hatopata ujira wa kusimama usiku mzima. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kusimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi huandikiwa ameswali usiku mzima.”[1]

Yote haya ni kwa ajili ya kutuhimiza kuchunga kubaki pamoja na imamu mpaka atakapomaliza. Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) waliafikiana na imamu wao katika jambo linalozidi juu ya kile kilichowekwa katika Shari´ah katika swalah moja. Hayo yalitokea pamoja na kiongozi wa waumini ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh) wakati aliposwali kikamilifu Minaa katika hajj. Aliswali Rak´ah nne licha ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Abu Bakr, ´Umar na ´Uthmaan mwenyewe mwanzoni mwa uongozi wake, mpaka kulipopita miaka minane, walikuwa wakiswali Rak´ah mbilimbili. Kisha baadaye akaswali Rak´ah nne. Maswahabah walimkemea jambo hilo. Pamoja na hivyo walikuwa wakimfuata na wakiswali pamoja naye Rak´ah nne. Basi ikiwa huu ndio mwongozo wa Maswhabah, nayo ni ile pupa ya kumfuata imamu, wana nini baadhi ya watu pindi wanapomuona imamu anazidisha juu ya ile idadi ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa hazidishi juu yake ambayo ni Rak´ah kumi na moja, basi  wanaondoka na kumwacha katikati ya swalah. Haya tunayashuhudia baadhi ya watu katika msikiti Mtakatifu wanaondoka kabla ya imamu kumaliza kwa hoja eti imamu amezidisha juu ya kile kilichosuniwa ambacho ni Rak´ah kumi na moja.

Tunasema kuwa kumfuata imamu ni jambo la lazima katika Shari´ah. Tofauti ni jambo la shari. Tofauti katika mambo ambayo inafaa kufanya Ijtihaad haitakiwi iwe ni chanzo cha makinzano na hitilafu kati ya Ummah khaswa ikiwa Salaf walitofautiana katika jambo hilo na katika suala hili hakuna dalili ya wazi inayozuia kufanya Ijtihaad.

Kwa hiyo ni lazima kwa mtu kujiepusha na uwongo, usengenyi, umbea, maneno ya haramu na matendo ya haramu akiwa amefunga. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule asiyeacha maneno ya kipuuzi na uongo, basi Allaah hana haja kwa yeye kuacha chakula na kinywaji chake.”

Kwa hiyo ni lazima kwa mfungaji achunge na aepuke mambo haya ya haramu na anatakiwa kujishughulisha kusoma Qur-aan katika Ramadhaan. Kwa sababu kuna sifa ya kipekee kusoma Qur-aan ndani ya Ramadhaan kwa sababu imeshuka ndani yake. Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijiliwa na Jibriyl ndani ya Ramadhaan na akimfunza Qur-aan. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati Jibriyl akimfunza Qur-aan alikuwa ni mkarimu zaidi katika mambo ya kheri kuliko upepo uliotumwa. Kwa msemo mwingine ni kwamba yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa anapoisoma Qur-aan basi inamwathiri kisha hapo ndio unaonekana ukarimu wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Katika mwezi huu tunapasa kutoa swadaqah kwa wingi. Kuna swadaqah sampuli mbili:

1 – Swadaqah ya wajibu. Nayo ni ile zakaah.

2 – Swadaqah iliyopendekeza. Nayo ni ile swaqadaqah ya mtu kujitolea mwenyewe.

Kwa hivyo toa swadaqah kwa wingi ndani ya mwezi huu kuwapa mafukara, masikini na wale watu wenye madeni na wengineo katika wahitaji. Kwani hakika swadaqah ndani ya mwezi huu ina sifa maalum ukilinganisha na miezi mingine.

Kuhusu zakaah ni swadaqah ya lazima. Nayo ni bora kuliko swadaqah iliyopendekezwa ya kujitolea. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika yale aliyopokea kutoka kwa Mola (´Azza wa Jall) ambaye amesema:

”Mja Wangu hatojikurubisha kwa chochote ninachokipenda zaidi kuliko yale niliyomfaradhishia.”[2]

Kwa ajili hii baadhi wanadhani kuwa mambo yaliyopendekezwa ni bora kuliko mambo ya faradhi. Mambo sivyo kabisa. Bali mambo ya faradhi ni bora kuliko yale mambo yaliyopendekezwa kutokana na Hadiyth hii. Endapo yangelikuwa si bora na yenye kupendeza zaidi mbele ya Allaah basi asingewafaradhishia nayo waja.

[1] Abu Daawuud (1375) na at-Tirmidhiy (806). Ni Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy.

[2] al-Bukhaariy (6502).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthyamiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Swalaat-it-Taraawiyh, uk. 06-8
  • Imechapishwa: 09/04/2022