Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ameuneemesha ummah huu – Allaah azidishe utukufu wake – kwa dini aliyoiridhia, nayo ni dini ya Uislamu, akamtuma kwao Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), mbora wa viumbe, na akamtukuza kwa Kitabu Chake, kilicho bora zaidi cha maneno. Amekusanya ndani yake (Subhaanahu wa Ta´ala) yote yanayohitajika katika khabari za waliotangulia na waliokuja baadaye, pamoja na mawaidha, mifano, adabu, aina mbalimbali za hukumu na hoja zilizo wazi na zenye kukata katika kuthibitisha upweke Wake na mengineyo miongoni mwa yale waliyokuja nayo Mitume Wake (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) yanayosambaratisha watu wa upinzani, upotovu na ujinga. Ameongeza malipo katika kuisoma, akatuamrisha kuipa umuhimu, kuitukuza, kushikamana na adabu zake na kujitahidi kwa uwezo wote katika kuitukuza.

Wanazuoni wengi miongoni mwa watu mashuhuri na wenye hadhi wameandika vitabu vinavyojulikana kuhusu fadhilah ya kusoma Qur-aan. Watu wa akili na busara wanavitambua vitabu hivyo, lakini ari zimepungua katika kuvihifadhi, sembuse kuvisoma, mpaka vikawa havinufaishi isipokuwa wachache miongoni mwa watu wenye ufahamu. Nimeona watu wa mji wetu wa Dameski – Allaah (Ta´ala) aulinde na auhifadhi pamoja na nchi zote za Uislamu – wakijishughulisha sana na kusoma Qur-aan Tukufu, wakijifunza nayo na kuifundisha, kuwasilisha na kujisomea, katika makundi na mmojammoja ambapo wakijitahidi katika hilo usiku na mchana – Allaah awazidishie juhudi juu yake na juu ya aina zote za utiifu – wakitaka uso wa Allaah wenye utukufu na ukarimu, jambo ambalo lilinifanya niweze kukusanya mukhtaswari kuhusu adabu za wanafunzi wenye kuibeba na sifa za wanaoihifadhi na wanaoitafuta.

Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amewajibisha kutoa nasaha kwa Kitabu Chake. Miongoni mwa nasaha hiyo ni kubainisha adabu za wabebaji wake na wanafunzi wake, kuwaongoza kwazo na kuwatanabahisha juu yake. Nimechagua kufupisha na nimejihadhari na kurefusha na kuzidisha. Katika kila mlango nimejitosheleza na sehemu ndogo yake na nimeashiria katika kutoa baadhi ya mifano ya baadhi ya adabu. Lengo langu ni kuashiria msingi wa jambo hilo na kuelekeza kwa ninachokitaja juu ya yale niliyoyaacha humo.

Sababu ya kuchagua kufupisha ni kwa kuwa ninapendelea kihifadhiwe, kiwe chenye kunufaisha sana na kuenea. Kisha yale majina mageni na lugha zitazotajwa ndani yake katika milango nimeyatenga kwa maelezo na ufafanuzi mfupi ulio wazi, kwa mpangilio mwishoni mwa kitabu ili mwenye kitabu anufaike kikamilifu na shaka iondoke kwa mtafutaji. Isitoshe katika milango yote kuna jumla ya kanuni na mambo ya thamani katika faida muhimu. Nimebainisha Hadiyth Swahiyh na dhaifu kwa kuzinasibisha kwa waliozipokea miongoni mwa maimamu wenye kuaminika. Wakati mwingine nimepuuza baadhi ya mambo machache katika hali fulani.

  • Muhusika: imaamImaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 16/08/2026