Ni ipi hukumu ya anayefanya kazi benki?

Swali: Ni ipi hukumu ya kufanya kazi katika mahakama zinazotumia sheria za kisekula? Kadhalika kufanya kazi katika mabenki ya ribaa kwa hoja kwamba ukiacha nafasi hiyo inaweza kuchukuliwa na wasiokuwa waislamu?

Jibu: Hili halijuzu. Ni lazima kuzuia ribaa, kutokukubaliana nayo na kujitahidi kutekeleza hukumu za Allaah zinazotokana na Shari´ah katika benki na katika taasisi zote. Inawajibika kwa dola za Kiislamu kulipa umuhimu mkubwa jambo hili na ziendeshe benki na taasisi za kifedha kwa hukumu za Allaah na zijitahidi kikamilifu ili benki katika nchi za Kiislamu ziende kwa mujibu wa Shari´ah ya Allaah na ribaa izuiwe kabisa bila kusita. Vilevile sheria za kisekula zinapaswa kupigwa marufuku isipokuwa zile zinazokubaliana na Shari´ah ya Allaah. Ni wajibu kwa dola za Kiislamu kuhukumu kwa Kitabu cha Mola wao na kwa Sunnah ya Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Wajihadhari wasifuate njia za maadui wa Allaah katika kutekeleza kanuni zinazoenda kinyume na Shari´ah. Hili ni miongoni mwa wajibu wao makubwa sana na hawana udhuru wowote kuhusu hilo. Ni wajibu kwao, kwa wajibu wa hakika, kuhukumu kwa Shari´ah ya Allaah ikiwa kweli wanadai kuwa ni waislamu. Ni lazima wahukumu kwa Shari´ah ya Allaah, wajitahidi pia kuyaendesha mabenki kwa misingi ya Kiislamu na kuyazuia miamala ya ribaa. Wanapaswa kuwashirikisha wanazuoni katika jambo hilo ili waweke misingi sahihi ya kuongoza benki na shughuli nyingine za kifedha ambazo watu huzifanya kinyume na Shari´ah.

Swali: Ni ipi hukumu ya kushiriki katika kazi hizi?

Jibu: Hili ni maasi makubwa na ni dhambi kubwa. Mtu akiyahalalisha mambo hayo, basi anakuwa kafiri. Mwenye kuhalalisha ribaa anakuwa kafiri. Mwenye kuhalalisha kuhukumu kwa yasiyoteremshwa na Allaah anakuwa kafiri. Lakini mtu anayefanya kwa sababu ya matamanio yake, huku akijua kuwa anafanya makosa, kwamba ni dhalimu na mwenye kuas, basi hakufuru kwa kitendo hicho. Atakuwa ni mtenda dhambi kubwa. Inampasa muislamu kumcha Allaah, awanasihi ndugu zake na awaongoze katika kheri.

Swali: Vipi kuhusu mtu anayefanya kazi katika benki?

Jibu: Haifai afanye kazi huko. Asishirikiane nao katika dhambi na uadui.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1103/حكم-العمل-في-البنوك-الربوية-والقضاء-بالقوانين-الوضعية
  • Imechapishwa: 16/08/2026