Himdi zote njema zote ni za Allaah, Mkarimu, Mwenye neema nyingi, Mwenye wingi wa fadhilah na ihsani, ambaye ametuongoza katika imani na akaifanya dini yetu kuwa bora kuliko dini zote na ametuneemesha kwa kumtuma kwetu kiumbe Wake mtukufu zaidi Kwake na aliye bora zaidi mbele Yake – mpenzi na kipenzi Chake wa hali ya juu, mja Wake na Mtume Wake Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa kupitia yeye akaondoa ´ibaadah za masanamu. Amemtukuza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Qur-aan, muujiza unaoendelea katika kupita kwa nyakati ambao anawapa changamoto nao wanadamu na majini wote kwa ujumla na kwa huo akawanyamazisha watu wote wa upotovu na ujeuri. Akaifanya kuwa chemchem ya nyoyo za watu wenye uoni wa ndani na maarifa. Hauchakai kwa kusomwa mara nyingi wala kwa kubadilika kwa nyakati. Ameifanya iwe rahisi kwa kukumbukwa mpaka watoto wadogo wakaihifadhi. Amehakikisha ulinzi wake kutokana na kuingia mabadiliko au mapya ndani yake. Imehifadhiwa, na sifa zote njema ni za Allaah na fadhilah Zake, muda wote usiku na mchana vinapobadilishana. Akawapa tawfiyq ya kujishughulisha na elimu zake wale aliowachagua miongoni mwa watu wa ustadi na umakini ambapo wakakusanya ndani yake kutoka kila fani yale yanayofurahisha nyoyo za watu wa yakini. Ninamhimidi kwa hayo na mengineyo katika neema Zake zisizohesabika, khaswa juu ya neema ya imani. Ninamuomba anijaalie mimi, wapendwa wangu na waislamu wote radhi Zake.

Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, ushahidi unaopatikana kwa kusamehewa, unaomuokoa mwenye nao na Moto na unaomfikisha kwenye makazi ya Pepo.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 12
  • Imechapishwa: 16/08/2026