Ndugu msomaji! Tambua ya kwamba mtunzi wa kijitabu “al-Iswaabah” ameandika kurasa mbili refu, uk. 14-15 kuhusiana na swalah ya ´Iyd sehemu ya uwanja ambapo wamejigonga wenyewe kwa njia ya kufedhehesha sana na imembainikia msomaji uchache wa elimu walionayo. Katika kitabu hicho wanatusemea uongo na kusema kwamba sisi hatuonelei kusihi kwa swalah ya ´iyd inayoswaliwa misikitini. Wamesema:

“Sababu iliyomfanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuchagua kuswali mahali pa uwanja ilikuwa ni kwa sababu hakukuwepo nafasi yenye kutosheleza Madiynah al-Munawwarah kutokana na kwamba katika mji hapakuwa isipokuwa msikiti mmoja tu.”

Huu ni ujinga uliyopindukia. Misikiti iliyokuwepo katika wakati wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa ni mingi na inayojulikana. Miongoni mwa misikiti iliokuwa maarufu ni msikiti wa Qubaa´, msikiti wa Qiblatayn na msikiti wa Fath. Kumekuja Hadiyth nyingi Swahiyh katika vitabu vya Sunnah kuhusiana na misikiti hii. Haafidhw katika “Fath-ul-Majiyd” (01/455) ametaja kwa majina misikiti mingine na anaweza kurejea huko yule anayetaka.

Malengo yao kwa kuleta madai haya batili ni kutaka kuitokomeza Sunnah ya kuswali swalah ya ´Iyd uwanjani. Ndio maana wakawa wameleta sababu hii ya uongo kwamba Madiynah hapakuwa isipokuwa msikiti wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tu. Isitoshe wanadai ya kwamba ulikuwa hauwatoshi waswalaji kuswali swalah ya ´Iyd! Lakini hata hivyo tumethibitisha ubatilifu wa sababu hii kwa kubatilisha madai kaunzia kwenye msingi wake. Hivyo basi tunasema endapo tukadirie kuwa msikiti wa Mtume ulikuwa hauwatoshi kuswali ndani yake, mtu anatakiwa kutambua kuwa kulikuwepo misikiti mingine mingi ambapo wangeliweza kuswalia, kama wafanyavyo watu hii leo. Kuacha kwao kuswalia ndani yake, na badala yake wakachagua kuswali uwanjani, ni dalili ya wazi kabisa yenye kuonesha kuwa Sunnah ni kuswali uwanjani pasi na misikiti. Makusudio yamethibitishwa na malengo yao ya utokomezaji yamebatilika.

Kisha wakasema:

“Wakati waislamu walipozidi kuwa wengi mpaka ikawa ni jambo lisilowezekana kwa waislamu kukusanyika sehemu ya uwanja, khaswa katika mji mkubwa kama Dameski, ndio wakakusanyika kwenye misikiti kutegemea na haja.”

Ndugu msomaji, tazama mantiki hii iliyo kinyume! Wanasema kuwa kuwakusanya waislamu sehemu ya uwanja ni vigumu, wakati ukweli wa mambo ni kwamba ni jambo sahali na ni rahisi. Dalili yenye kuthibitisha hilo, ni kwamba miji mingi ilikuwa ni yenye kufanya hivo, kama alivosema an-Nawawiy kwenye “Sharh Swahiyh Muslim”. Himdi zote ni za Allaah kuona Sunnah hii mpaka hii leo inatendewa kazi katika miji mingi ya Kiislamu kama vile Dameski, Jordan, Misri, Algeria, Hijaaz, Pakistan na mingineyo.

Isitoshe kuna faida gani ya kufarikisha mkusanyiko wa waislamu kwa misikiti yote hii iliokaribiana, ambayo wakati mwingine mtu hupigi tambo khamsini kutoka kwenye msikiti mmoja hadi mwingine? Lau waandishi hawa wangeliyafungamanisha maneno yao kwa kuswali kwenye msikiti mmoja tu mkubwa, wangelikuwa na aliyewatangulia katika hili, kama itakavyokuja kuhusu Imaam ash-Shaafi´iy (Rahimahu Allaah). Lakini watu hawa wao hawaoni neno kusema kitu ambacho hakikusemwa na muislamu yeyote kabla yao pale wanapoipiga vita Sunnah. Vinginevyo waislamu wote wameafikiana juu ya kwamba Sunnah ni kuswali sehemu ya uwanja ikiwa msikiti haukuwatosha. Uhakika wa mambo ni kwamba wengi hawakukubali sharti hii, bali wamesema kuwa swalah inatakiwa kuswaliwa sehemu ya uwanja hata kama watapata nafasi ya kutosha msikitini. Kutokana na ujinga wao wamekwenda kinyume na waislamu wote, wale wa kale na wale waliokuja nyuma, ilihali Allaah (Ta´ala) amesema:

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Atakayempinga Mtume baada ya kuwa imekwishambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi Tutamgeuza alikogeukia na tutamwingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kuishia!”[1]

Enyi watu, ala ala shikamaneni na Sunnah!

[1] 04:115

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swalaat-ul-´Iydayn, uk. 4-8
  • Imechapishwa: 12/05/2020