31 – Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake anapokuwa amesujudu. Hivyo basi, ombeni du´aa kwa wingi.”[1]

Ameipokea Muslim.

32 – Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ameeleza kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ama katika Sujuud jitahidini katika du´aa. Kuna matumaini makubwa na nyinyi kuitikiwa.”[2]

Ameipokea Muslim.

MAELEZO

Hadiyth hizi mbili zinafahamisha kuwa inapendeza kuomba du´aa kwa wingi katika sujuud. Mja anakuwa karibu zaidi na Mola wake wakati amesujudu. Kwa ajili hiyo amesema (Subhaanah):

وَاسْجُدْ وَاقْتَرِب

”Basi sujudu na kurubia.”[3]

Kwa sababu mja anapiga uso wake, paji la uso na pua yake kwenye udongo juu ya ardhi. Hili hafanyiwi mwingine isipokuwa tu Yeye (Subhaanah). Ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema:

“Ama katika Sujuud jitahidini katika du´aa. Kuna matumaini makubwa na nyinyi kuitikiwa.”

Bi maana kuna uhakika mkubwa wa nyinyi kuitikiwa.

[1] Muslim (482).

[2] Muslim (479).

[3] 96:19

  • Muhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ad´iyah wal-Adhkaar, uk. 37
  • Imechapishwa: 07/10/2025