1 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Abu Mu´aawiyah ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa Saalim bin Abiyl-Ja´d, ambaye ameeleza ya kwamba Mtume wa Allaah  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika miongoni mwa ummah wangu yuko ambaye lau ataenda mlango wa mmoja wenu na kumwomba dinari hatompa, na lau atamwomba dirhamu hatompa. Lau atamwomba Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) Pepo atampa, lakini endapo atamwomba ulimwengu hatompa nayo, hata hivyo si kwamba amemnyima nayo kwa sababu ya kumdharau. Mtu mwenye nguo mbili zilizopasuka. Iwapo ataapa kwa Allaah (´Azza wa Jall) basi atamtimizia.”[1]

2 – Muhammad bin ´Abdil-Wahhaab ametuhadithia: Ya´quub al-Qummiy ametuhadithia, kutoka kwa Ja´far bin Abiyl-Mughiyrah, kutoka kwa Sa´iyd bin Jubayr, kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ambaye amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alimtembelea bwana mmoja mgonjwa wa Wanusuraji. Wakati alipokaribia katika nyumba yake akamsikia akizungumza ndani. Lakini alipoingia hakuona mtu yeyote. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Nimekusikia ukiongea na mtu mwingine.” Akasema: “Ee Mtume wa Allaah, nimeingia ndani kwa sababu ya kuumizwa na maneno ya watu juu ya homa nilionayo. Kisha akaingia kwangu mwanaume ambaye sijawahi kumuona mtu yeyote baada yako mwenye tabia nzuri na mwenye maneno mazuri kama yeye.” Akasema: “Huyo alikuwa Jibriyl. Hakika miongoni mwenu kuna watu ambao ikiwa mmoja wao atamwapia Allaah (´Azza wa Jall) kwa kiapo, basi atamtimizia.”[2]

3 – ´Abdur-Rahmaan bin Swaalih ametuhadithia: Ismaa´iyl bin ´Ayyaash ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Muhaajir al-Answaariy, kutoka kwa al-´Abbaas bin Saalim al-Lakhmiy, ambaye amesema:

”´Umar bin ´Abdul-´Aziyz alimtuma mjumbe kwenda kwa Abu Sallaam al-Habashiy, akabebwa juu ya kipando. Alipoingia kwake akamwambia: ”Hakika ulinisumbua (au alisema ”Hakika umesumbua miguu yangu”).” ´Umar akamwambia: ”Hatukukusudia hivyo, lakini nimefikiwa kutoka kwako na Hadiyth ya Thawbaan kuhusu Hodhi na hivyo ndio nikapenda kuzungumza nawe uso kwa uso.” Akasema: ”Nimemsikia Thawbaan akisema: Nimemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

”Hakika Hodhi yangu mwendo wake ni kutoka ´Adan mpaka ´Ammaan al-Balqa´. Maji yake meupe zaidi kuliko maziwa na matamu zaidi kuliko asali. Vikombe vyake ni idadi ya nyota za mbinguni. Atakayekunywa humo funda moja hatatoka kiu baada yake milele. Wa kwanza kufika hapo ni mafakukara wa Wahajiri.” ´Umar bin al-Khatwaab akasema: ”Ni kina nani hao, ee Mtume wa Allaah?” Akasema: ”Hao ni wale wenye nyweletimtim na nguo zao chafu. Hawaoi wanawake wanaojistarehesha na wala hawafunguliwi milango ya viongozi.” ´Umar bin ´Abdul-´Aziyz akasema: ”Kwa hakika mimi nimefunguliwa milango ya viongozi na nimeoa wanawake wanaojistarehesha. Basi sitapaka mafuta kichwani mwangu mpaka ziwe timtim, wala sitasafisha nguo yangu inayogusa mwili wangu mpaka ichafuke.”[3]

4 – Ishaaq bin Ismaa´iyl ametuhadithia: Sufyaan ametuhadithia, kutoka kwa Muhammad bin Suuuqah, aliyesema:

”Waislamu walizunguka ngome katika ngome za maadui, walipokuwa katika hali hiyo walimuona bwana mmoja. Baadhi yao wakawaambia wengine: ”Ee fulani, kama kwamba huyu ana sifa alizoelezea Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati alipozungumzia kuhusu mtu mwenye nywele timtim na mwenye mavazi mawili ya zamani.” Wakamwambia mmoja wao: ”Zungumza naye.” Basi akazungumza naye na wakamwomba amwombe du´aa Allaah (´Azza wa Jall) afungue ngome hiyo. Akamuomba Allaah ambapo akaifungua.”

[1] Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (1863).

[2] Cheni za wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-Haythamiy katika “Majma´-uz-Zawaa’id” (10/41).

[3] at-Tirmidhiy (2444). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (2444).

  • Muhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiyd-Dunyaa (afk. 281)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Khumuul wat-Tawaadhwu´, uk. 15-23
  • Imechapishwa: 21/01/2026