01. Swawm ya aliyetwahirika punde tu baada ya alfajiri

Swali 1: Mwanamke akisafika papohapo baada ya alfajiri ajizuie na kufunga siku hiyo? Anahesabiwa siku hiyo au ni lazima kwake kulipa siku hiyo?

Jibu: Mwanamke akisafika baada ya kuchomoza kwa alfajiri wanachuoni wana maoni mawili juu ya kujizuia:

1 – Ni lazima kwake kujizuia masaa yaliyobaki ya siku hiyo. Siku hiyo haihasabiki kwake. Bali ni lazima kwake kuilipa. Maoni haya ndio yametangaa katika madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah).

2 – Si lazima kujizuia masaa yaliyobaki ya siku hiyo. Kwa sababu siku hiyo haisihi kufunga ndani yake kwa sababu mwanzoni mwake alikuwa ni mwenye hedhi na hakuwa miongoni mwa wafungaji. Ikiwa siku hiyo haisihi basi kujizuia hakuna faida yoyote. Kipindi hichi si chenye kuheshimika kwa nisba yake. Kwa sababu ameamrishwa kula mwanzoni mwa mchana. Bali imeharamishwa kwake kufunga mwanzoni mwa mchana. Swawm iliyowekwa katika Shari´ah ni kule mtu kujizuia na vifunguzi hali ya kumwabudu Allaah kuanzia kuchomoza kwa alfajiri mpaka kuzama kwa jua. Maoni haya – kama unavyojionea mwenyewe – ndio yenye nguvu zaidi kuliko maoni yanayomlazimisha kujizuia. Pasi na kujali ni maoni gani anayochukua ni lazima kwake kuilipa siku hii.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 60 su-aal wa jawaab fiy Ahkaam-il-Haydhw, uk. 7-8
  • Imechapishwa: 04/06/2021