01. Sababu ya wanazuoni kupatiliza vitabu vya ´Aqiydah

Himdi zote njema zinamstahikia Allaah. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Haya ni maelezo ya mashairi ya Abu Bakr bin Abiy Daawuud as-Sijistaaniy (Rahimahumaa Allaah). Ndani yake mna ´Aqiydah yake na yale anayoonelea na kwamba ni mwenye kuwafuata Salaf katika hayo.

Waislamu katika kizazi cha kwanza, kuanzia karne za Maswahabah na karne bora zilizokuja baada yao, walikuwa wakiamini yaliyomo katika Qur-aan na Sunnah pasi na kuwa na kutilia mashaka. Kwa sababu walikuwa ni wenye kumuamini Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) imani ya kweli na yenye nguvu. Hivyo wakaamini yaliyokuja katika Qur-aan na Sunnah. Kila kilichomo ndani ya Qur-aan, Sunnah na mambo yote ya dini walikuwa ni wenye kuyaamini. Hawakuwa ni wenye kuyatilia shaka. Ni mamoja yawe yanahusiana na mambo ya ´Aqiydah, ´ibaadah, biashara, adabu, tabia na hukumu mbalimbali za Kishari´ah za halali na haramu. Hawakuwa wanakomeka juu ya kitu katika hayo. Kwa kuwa imani inapelekea hivo. Walikuwa wameamini kihaki na kikweli. Hawakuwa na mashaka kwa yale yaliyothibiti katika Qur-aan na Sunnah katika maudhui yote na katika maelezo yake juu ya mambo yaliyopita na yaliyoko mbele. Hawakuwa wanabagua chochote katika mambo yaliyotajwa ndani ya Qur-aan na Sunnah isipokuwa wanakiamini imani ya kukata kabisa. Hivi ndivyo inavyopelekea imani.

Baadaye mwishoni mwa zama za Maswahabah kukajitokeza mapote potevu. Kwa mfano Khawaarij, Shiy´ah, Murji-ah na Qadariyyah. Haya ndio mapote yaliyodhihiri. Wakati wa karne bora wenye nayo walikuwa wanajificha na hawafichui uendaji kinyume huu. Ilikuwa yule ambaye anafichua kitu katika hayo basi anachukuliwa hatua na kukemewa. Endapo anafikia katika kiwango cha kuritadi basi alikuwa anauawa ili kuilinda dini hii isije kuchezewa na wachezaji hawa. Pindi karne bora ziliisha na kukaingia tamaduni za kigeni katika miji ya Kiislamu. Mfano wa tamaduni hizo ilikuwa ni za kirumi na wagiriki. Hapo ndipo kukatokea kasoro na walinganizi wa upotevu wakapata uchangamfu kueneza upotevu huu. Kuanzia wakati huo ndio wanazuoni nao wakapata uchangamfu wa kubainisha ´Aqiydah ya  Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah iliokuwa ikifuatwa na Maswahabah wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), wanafunzi wa Maswahabah na waliokuja baada wanafunzi wa Maswahabah. Wakaiandika ´Aqiydah hiyo kwenye vitabu. Kipindi hicho walikuwa wakiita “Iymaan”, “ash-Shariy´ah”, “as-Sunnah” na “Tawhiyd”. Wakaiandika wakiwaraddi wenye kwenda kinyume. Hilo ni kutokana na upole wa Allaah juu ya Ummah huu ili dini yao iweze kubaki. Allaah katika kila zama huwateua walinzi ili wailinde. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah ambaye amefanya katika kila zama kuwepo wanazuoni katika kipindi na kusita ujio wa Mitume. Wanawalingania waliopotea katika uongofu na wanasubiri juu ya maudhui yao. Wanahuisha kwa Kitabu cha Allaah wale wafu, na wanawafanya kuweza kuona kwa nuru ya Allaah wale vipofu. Ni wangapi waliouliwa na Ibliys wamewahuisha! Ni wapotofu wangapi waliodanga ambao wamewaongoza! Ni athari nzuri iliyoje walionao kwa watu na ni ubaya uliyoje athari ya watu dhidi yao! Wanakilinda Kitabu cha Allaah upotoshaji wa waliochupa mipaka, madai ya watu wa batili na upindishaji wa maana wa wajinga; watu ambao wamechochewa kwa bendera za Bid´ah na kufungua njia za fitina. Wametofautiana juu ya Kitabu, wanaenda kinyume na Kitabu na wamkusanyika juu ya kufarikiana na Kitabu. Wanasema juu ya Allaah na juu ya Kitabu cha Allaah pasi na elimu. Wanazungumza maneno yasiyokuwa wazi na wanawahaa wajinga katika watu katika wanayowababaisha. Tunamuomba Allaah ulinzi kutokana na fitina zinazopotosha.”[1]

Baada ya hapo waislamu wakarithi vitabu hivi na wakafupisha vitabu vya ´Aqiydah. Wakarithishana vitabu hivi vilivyotungwa na maimamu hawa. Ndipo kukapatikana vitabu vya ´Aqiydah ambavyo ndani yake mlikuwa mambo yote yanayohusiana na ´Aqiydah waliokuwa wakifuata Salaf wa Ummah huu. Baadhi ya wanazuoni wakatilia umuhimu kuviweka vitabu hivi kwa mtindo wa mashairi. Kwa sababu vitabu vilivyo kwa mtindo wa mashairi ni vyepesi na vinahifadhika haraka na vinabaki kwenye kumbukumbu. Ndipo wakatunga vitabu hivi vinavyozungumzia ´Aqiydah ili iwe sahali kuvihifadhi. Miongoni mwavyo ni shairi hili liliyoko mbele yetu kwa jina “Haa-iyyah” ya Ibn Abiy Daawuud.

[1] ar-Radd ´alaal-Jahmiyyah waz-Zanaadiqah, uk. 85

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Mandhuumat-ul-Haaiyyah fiy ´Aqiydati Ahl-is-Sunnah wal-Jamaa´ah, uk. 43-45
  • Imechapishwa: 16/12/2023