01. Sababu ya kwanza ya maisha mazuri: Imani

1- Sababu kubwa zaidi ya hilo, msingi wake na asili yake ni imani na matendo mema. Amesema (Ta´ala):

مَنْ عَمِلَ صَالِحًا مِّن ذَكَرٍ أَوْ أُنثَىٰ وَهُوَ مُؤْمِنٌ فَلَنُحْيِيَنَّهُ حَيَاةً طَيِّبَةً ۖ وَلَنَجْزِيَنَّهُمْ أَجْرَهُم بِأَحْسَنِ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ

“Yule mwenye kutenda mema katika wanamme au wanawake – ilihali ni muumini – basi Tutamhuisha maisha mazuri na tutawalipa ujira wao kwa mazuri zaidi ya yale waliyokuwa wakitenda.”[1]

Amekhabarisha (Ta´ala) na akaahidi kwa yule mwenye kukusanya kati ya imani na matendo mema kumpa maisha mazuri katika dunia hii na malipo mazuri huko Peponi. Sababu ya hayo iko wazi: kumwami Allaah imani sahihi inayozalisha matendo mema inayozitengeneza nyoyo, tabia, dunia na Aakhirah. Wana msingi ambao kwao wanayapokea yale yote yanawajia katika sababu za furaha na sababu za dhiki, msongo wa mawazo na huzuni.

Wanayapokea wanayoyapenda na yenye kufurahisha kwa kuyakubali, kuyashukuru na kuyatumia katika yale yanayonufaisha. Wakiyatumia kwa njia hii basi wanaruzukiwa na jambo la kufurahika nayo, kutamani kubakia kwake na baraka zake, kutaraji thawabu za wale wenye kushukuru, mambo makubwa ambayo kheri na baraka zake zinashinda furaha hizi ambazo ndio matunda yake.

Mambo yenye kuchukiza, yenye kukera wanayapokea, msongo wa mawazo na ya kusononesha wanayapokea kwa kule kupambana nayo kwa kila kinachowezesha kupambana nayo katika kuyafanya mepesi kwa kiasi inavowezekana na subira njema ambayo ni lazima kwao. Kwa njia hiyo kunapatikana kwao kutokana na zile athari za mabaya yaliyowafika kupambana nayo kwa mambo yenye manufaa, uzoefu, nguvu, subira na kutaraji malipo kutoka kwa Allaah, mambo makubwa yanayoondosha yale yanayochukiza. Inachukua nafasi yake furaha, matarajio mazuri, kutamani fadhilah na thawabu za Allaah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema katika Hadiyth Swahiyh:

“Ajabu iliyoje juu ya jambo la muumini. Hakika mambo yake yote huwa ni kheri. Asifikwa na kitu cha kufurahisha basi hushukuru na ikawa ni kheri kwake. Na akifikwa na kitu cha kusononesha basi husubiri na ikawa ni kheri kwake – na hilo haliwi kwa yeyote isipokuwa kwa muumini tu.”[2]

Hivyo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akaeleza kwamba muumini inaongezeka ngawira, kheri na matunda ya matendo yake katika kila kinachompata katika ya kufurahisha na kuchukiza. Kwa ajili hiyo utaona watu wawili waliofikwa na jambo la kufurahisha au la kuchukiza lakini hata hivyo wakatofautiana utofauti mkubwa katika kule kuyapokea kutegemea na kule kutofautiana kwao katika imani na matendo mema.

Wale wenye kusifika kwa sifa mbili hizi wanaipokea kheri na shari kwa yale tuliyoyataja katika shukurani, subira na yale yanayohusiana nayo. Matokeo yake yanamletea furaha, tabasamu na kuondoka kwa misononeko, msongo wa mawazo, kifua chenye dhiki, maisha ya tabu na maisha mazuri yanakamilika juu yake katika dunia hii.

[1] 16:97

[2] Muslim.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Wasaa-il-ul-Mufiydah lil-Hayaat-is-Sa´iydah, uk. 12-14
  • Imechapishwa: 08/06/2020