01. Sababu ya kuandikwa kitabu ”Bard-ul-Akbaad ´indaa Faqd-il-Awlaad”

Himdi zote njema zinamstahikia Allaah Hakimu Mwenye hekima katika yale anayoyakadiria na kuyahukumu, Muweza na Mwenye kushinda katika amri Zake anazozitekeleza. Yule mwenye kuyaridhia, basi humtunuku na kumfurahisha, na yule mwenye kuyakasirikia, basi hatopata jingine isipokuwa hasira – mtu kama huyo atawekwa na kufukuzwa mbali. Maangamivu ni kwa wale ambao wanakasirikia hukumu Yake na kuchukizwa na hukumu Zake, pongezi kwa wale ambao wanajisalimisha kwa matendo Yake, wananyenyekea makadirio Yake na kwa hali zote wanafurahikia na kusema:

إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea – hao zitakuwa juu yao baraka kutoka kwa Mola wao na rehema na hao ndio wenye kuongoka.”[1]

Tunamuhimidi Allaah kutokana na yale makadirio matamu na machungu. Tunamshukuru daima kutokana na zile amri Zake anazozipitisha. Tunashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika – shahaadah inayoshuhudiwa na ambaye ana subira katika misiba yake na mwenye kuyakinisha yale malipo makubwa ambayo Allaah ameahidi juu ya subira na adhabu kali juu ya kughadhibika – na nashuhudia ya kwamba bwana wetu Muhammad ni mja na Mtume Wake mwaminifu ambaye kifo chake kimefanywa ni liwazo kwa kila muislamu mwenye kuhuzunika na ambaye Amemteremshia ndani ya Kitabu Chake kilichohifadhiwa:

إِنَّكَ مَيِّتٌ وَإِنَّهُم مَّيِّتُونَ

“Hakika wewe utakufa na wao pia ni watakufa.”[2]

Allaah amsifu na amsalimishe yeye, jamaa zake, wenye heshima na fakhari kubwa na Maswahabah wake wenye ngazi za juu na busara.

Huu ni ukumbusho kwa wale wenye busara na ni liwazo kwa kila muumini ambaye amepatwa na msiba. Utafungua kifua chake, kuleta subira yake, kusahilisha hali yake, kukhafifisha jambo lake na kumfahamisha malipo yake juu ya subira yake. Nimekiandika harakaharaka mwanzoni mwa Shawwaal kutokana na mazingira yalivyokuwa. Kwa sababu nilipokuwa na khabari ya kwamba kuna mtoto aliyeaga dunia wa bwana mmoja mwema na ndugu mwenye kuheshimika – Allaah ayafanye makubwa malipo yake kutokana na msiba wake na asimnyime malipo yake makubwa, amfanye awe ni mwenye kujisalimisha juu ya amri Yake, kuridhia makadirio Yake matamu na machungu, ampe badala ya mtoto aliyeaga dunia aliye bora zaidi na amfanyie upole kama alivowafanyia upole wale wema katika Salaf.

[1] 2:156-157

[2] 39:30

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin ´Abdillaah bin Naaswir-id-Diyn ad-Dimashqiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Bard-ul-Akbaad ´inda Faqd-il-Awlaad, uk. 27-28
  • Imechapishwa: 08/08/2023