01. Picha – haramu iliyo kubwa

Himdi zote njema anastahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na salamu zimshukie bwana wetu Muhammad, na jamaa zake watwaharifu.

Ama baada ya hayo;

Hakika nimefikiwa na swali kutoka kwa muheshimiwa ´Allaamah Jamaal al-Kamaal ‘Aliy bin Yahyaa. Swali lenyewe ni kama ifuatavyo: Makatazo yamesihi au hapana? Baada ya kusihi katazo hilo, je, linachukuliwa kuwa ni haramu au ni machukizo? Baada ya kulichukulia katika mojawapo ya hukumu hizo mbili, je, katazo hilo linahusu baadhi ya vitu pekee bila vingine au linahusu vyote? Je, jambo hili ni miongoni mwa yale yanayopaswa kukemewa au hapana?

Swali hili limekusanya masuala manne. La kwanza: Je, katazo la picha limesihi au hapana?

Hakika kumesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) katika jambo hili yale yaliyo makubwa zaidi kuliko katazo la kawaida na yenye kuonesha wazi uharamu wake, nayo ni onyo la watengenezaji pciha kwamba kwa Moto. al-Bukhaariy, Muslim na wengineo wamepokea kwamba Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anh) amesema ameeleza kuwa amemsikia Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) akisema:

“Kila mtengeneza pica yuko Motoni. Atafanywa kwa kila picha aliyotengeneza aiweke roho, ambayo ataadhibiwa kwayo ndani ya Jahannam.” Ikiwa ni lazima ufanye, basi chora miti na vitu visivyo na roho.”[1]

al-Bukhaariy, Muslim na wengineo wamepokea kwamba Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhumaa) ameeleza kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Wale wanaotengeneza picha hizi wataadhibiwa siku ya Qiyaamah, ambapo wataambiwa: ”Fufueni mlivyoviumba!”[2]

al-Bukhaariy, Muslim na wengineo wamepokea kwamba ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema:

”Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) alirudi kutoka safarini. Nami nilikuwa nimefunika sehemu chumbani mwangu kwa pazia lenye michoro ya viumbe. Alipoliona alilirarua na uso wake ukabadilika ambapo akasema: “Ee ‘Aaishah! Hakika watu wenye adhabu kali zaidi siku ya Qiyaamah ni wale wanaofananisha uumbaji wa Allaah.” Tukaikata na tukafanya baadaye mto mmoja au mito miwili.”[3]

al-Bukhaariy, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy wamepokea kwamba Ibn ‘Abbaas kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote atakayetengeneza picha, basi Allaah atamuadhibu kwayo siku ya Qiyaamah mpaka apulize roho ndani yake, kitu ambacho hatoweza kukifanya.”[4]

Hizi Hadiyth zinaonesha wazi kwamba watengeneza picha wataadhibiwa Motoni, jambo ambalo ni katika dalili kubwa kabisa zinazofahamisha uharamu wa jambo hili. Kwa sababu hakuna kinachopelekea kuadhibiwa Motoni isipokuwa kwa jambo lililoharamishwa kwa mujibu wa Shari´ah. Isitoshe dalili hizi zinaonesha uharamu kwa nguvu zaidi kuliko katazo la kawaida. Kwa sababu katazo linaweza kuhamishwa kutoka maana yake ya asili kwenda maana ya machukizo kwa sababu ya dalili fulani, kama ilivyothibitishwa katika misingi ya Fiqh. Lakini onyo la Moto haliwezi kugeuzwa; linafahamisha uharamu kwa dalili iliyo wazi na haliondolewi isipokuwa kwa dalili inayothibitisha kufutwa kwake.

[1] al-Bukhaariy (2225) na Muslim (2110).

[2] al-Bukhaariy (5951 na 7558) na Muslim (2108).

[3] al-Bukhaariy (5954) na Muslim (2107).

[4] al-Bukhaariy (5963) na Muslim (2110).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin ´Aliy ash-Shawkaaniy (afk. 1250)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Hukm-ut-Taswwiyr, uk. 13-18
  • Imechapishwa: 05/05/2026