01. Maana ya swawm kilugha na kwa mujibu wa Shari´ah

Maana ya swawm kwa mujibu wa lugha ni kule kujizuia. Husemwa kuwa jua limefunga pale linaposimama. Ambaye ananyamaza huambiwa kuwa amefunga pale anapojizuilia kuongea. Amesema (Ta´ala) kuhusu Maryam (Radhiya Allaahu ´anhaa):

إِنِّي نَذَرْتُ لِلرَّحْمَـٰنِ صَوْمًا فَلَنْ أُكَلِّمَ الْيَوْمَ إِنسِيًّا

“Hakika mimi nimeweka nadhiri kwa Mwingi wa rehema ya kujizuia [na kusema], hivyo basi leo sitomsemesha mtu yeyote.”[1]

Bi maana tumefunga kwa sababu tumejizuilia kuongea. Farasi aliyegoma kutembea huambiwa kuwa amefunga.

Imekuja katika ”al-Qaamuus”:

”Swawm ni kule kujizuilia na chakula, kunywa, kuzungumza, tendo la ndoa na kutembea.”[2]

al-Fayuumiy amesema:

”Kumesemwa kuwa swawm kwa mujibu wa lugha ni kule kujizuilia kwa moja kwa moja… ”

Abu ´Ubaydah amesema:

”Kila mwenye kujizuilia na chakula, kuzungumza na kutembea basi amefunga.”[3]

al-Khaliyl amesema:

”Swawm ni kusimama bila kutenda.”

Swawm kwa mujibu wa Shari´ah ni kujizuilia kwa manuizi kutokana na vitu kutoka kwa mtu maalum na kwa sharti maalum[4].

[1] 19:26

[2] al-Qaamuus (01/1131). Tazama pia ”al-Maghrib” (247) ya al-Matwriziy.

[3] Tazama ”al-Iswbaah al-Muniyr” (352).

[4] Tazama ”al-Maghniy” (03/104) ya Ibn Qudaamah na ”ar-Rawdhwa al-Murbiy´ Sharh Zaad-ul-Mustaqniy” (01/225).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Ilmaam bishay´ min Ahkaam-is-Swiyaam, uk. 07-08
  • Imechapishwa: 23/03/2023