01. Maafikiano ya waislamu kwa kuwepo Allaah juu ya viumbe Wake

Himdi zote zinamstahikia Allaah ambaye kalingana juu ya mbingu Zake na akajionyesha kwa yakini nyoyoni mwa mawalii Wake. Amewapangia katika makadirio Yake na akawabariki katika hukumu Zake. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika, kama shahaadah ya ambaye anaamini kukutana Naye, na nashuhudia ya kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni mja, Mtume na Nabii wake wa mwisho.

Amma ba´d:

Allaah (Ta´ala) amejieleza Mwenyewe ya kwamba amelingana juu mbinguni. Kadhalika Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ambaye ndiye Mtume wake wa mwisho, amemweleza hivo. Wanachuoni wote katika wale Maswahabah wachaji na maimamu mabingwa wakaafikiana juu ya hilo. Kumepokelewa mapokezi mengi kabisa juu ya hilo kwa njia inayopelekea katika yakini. Allaah (Ta´ala) amezikusanya nyoyo za waislamu juu ya hilo na akaliweka katika maumbile ya viumbe wote. Wakati wa matatizo utawaona namna wanavyotazama juu mbinguni na wanazielekeza du´aa zao na mikono yao mbinguni. Wanasubiri Mola wao awaokoe na wanayasema hayo wazi wazi kwa kinywa kipana. Hakuna yeyote anayepinga hayo isipokuwa tu mtu wa Bid´ah au aliyepewa mtihani mfuata kichwa mchunga anayefuata upotevu wake.

Hapa nitataja baadhi ya mapokezi juu ya hilo yaliyonifikia kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah wake na maimamu wa kale. Wameyapokea kwa njia ya kukata mashauri kabisa na ya yakini juu ya usahihi wake. Kuna mapokezi mengi kabisa kutoka kwao na wingi wake unajulikana. Lengo ni ili wale waumini watakaoyasoma imani yao iweze kupanda na wazinduke kwa yale yaliyozoeleka kuwa ni yenye kufichikana kwao, ili aweze kuielewa mada yenyewe na kushikamana bara bara na dalili na hoja.

  • Mhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithbaatu Swifat-il-´Uluww, uk. 63
  • Imechapishwa: 10/02/2017