01. Kuna vifunguzi vingapi vinamfunguza mfungaji?


Swali 1: Ni vifunguzi vipi vinavyomfunguza mfungaji?

Jibu: Vifunguzi ndani ya Qur-aan ni vitatu:

1 – Kula.

2 – Kunywa.

3 – Jimaa.

Dalili ya hayo ni maneno Yake (Ta´ala):

فَالْآنَ بَاشِرُوهُنَّ وَابْتَغُوا مَا كَتَبَ اللَّـهُ لَكُمْ ۚ وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِۖ ثُمَّ أَتِمُّوا الصِّيَامَ إِلَى اللَّيْلِ

“Basi sasa changanyikeni nao [waingilieni] na tafuteni Aliyokuandikieni Allaah kwenu. Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu weupe wa alfajiri katika weusi wa usiku. Kisha timizeni swawm mpaka usiku.”[1]

Kwa nisba ya kula na kunywa ni mamoja kitu hicho ni halali au haramu. Ni mamoja pia kiwe ni chenye kunufaisha au chenye kudhuru, au si chenye kudhuru wala chenye kunufaisha. Vilevile ni mamoja kiwe kidogo au kikubwa. Kujengea juu ya haya uvutaji sigara unafunguza ingawa ni yenye kudhuru na ni haramu. Wanachuoni wamefikia mpaka kusema kwamba ikiwa mtu atameza lulu basi amefungua. Lulu hainufaishi kitu mwili lakini pamoja na hivyo inazingatiwa ni katika vyenye kufunguza. Lau atakula unga uliochanganyikana na najisi anakuwa mwenye kufungua pamoja na kwamba ni wenye kudhuru.

Tatu ni jimaa ambayo ndio kifunguzi kikali zaidi kutokana na ile kafara inayolazimika juu yake. Kafara ni kuacha mtumwa huru. Asipopata basi atatakiwa kufunga miezi miwili mfululizo. Asipoweza basi atatakiwa kufunga siku sitini.

Nne ni kujitoa manii kwa ladha. Mtu akijitoa manii kwa ladha basi ameiharibu funga yake. Lakini hatohitajia kutoa kafara. Kwa sababu kafara inakuwa katika jimaa peke yake.

Tano ni sindano zinazomtosheleza mtu kutohitaji chakula. Nazo ni zile sindano za lishe. Kuhusu sindano za kawaida haziharibu funga. Ni mamoja imedungwa kwenye mshipa wa koo au kwenye misuli. Kwa sababu sio kula wala kunywa wala hakuna maana ya kula na kunywa.

Sita kujitapisha. Mtu akijitapisha makusudi swawm yake inaharibika. Lakini hana kitu endapo matapishi yatamshinda.

Saba kutokwa na hedhi na nifasi. Mwanamke akitokwa na hedhi na damu ya uzazi, japo muda mdogo kabla ya kuzama kwa jua, basi swawm yake inaharibika. Na damu ya uzazi au ya hedhi ikimtoka baada ya kuzama kwa jua, ijapo muda mdogo tu baada ya kuzama kwa jua, funga yake ni yenye kusihi.

Nane kuumikwa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Anayefanya na anayefanyiwa chuku wametengua swawm.”[2]

Mtu akiumikwa na kukaonekana damu basi swawm yake inaharibika kutokana na chuku yake ikiwa imetumiwa ile njia iliokuwa inatambulika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nayo ni kwamba mfanya chuku anavuta damu kwa vichupa. Ama akifanya chuku kwa mashine iliojitenga na yule mfanya chuku, basi hakika mwenye kuumikwa amefungua na mwenye kuumika hakufungua.

Vifunguzi hivi vikimtokea mfungaji mchana wa Ramadhaan kipindi cha funga yake atalazimika kulipa. Isitoshe kitendo hicho kitapelekea katika mambo manne:

1 – Dhambi.

2 – Kuharibika kwa funga.

3 – Ulazima wa kujizuia sehemu iliobaki ya siku hiyo.

4 – Ulazima wa kulipa.

Ikiwa kufungua kumetokana na jimaa basi hilo litapelekea katika jambo la tano ambalo ni ile kafara.

Lakini tunapaswa kutambua kwamba vifunguzi hivi haviharibu funga isipokuwa kwa sharti tatu:

1 – Ujuzi.

2 – Kukumbuka.

3 – Matakwa.

Mfungaji akitumia chochote katika vifunguzi hivi pasi na kujua, basi funga yake ni sahihi. Ni mamoja alikuwa hajui wakati au alikuwa hajui hukumu.

Mfano wa ambaye alikuwa hajui wakati ni mtu kuamka mwishoni mwa usiku huku akidhani kuwa hakujachomoza alfajiri na hivyo akala na kunywa na baadaye ikambainikia kuwa alfajiri ilikuwa imekwishachomoza, huyu funga yake ni sahihi kwa sababu alikuwa ni mjinga wa wakati.

Mfano wa ambaye alikuwa hajui hukumu ni mfungaji kufanya chuku na huku hajui kuwa kufanya chuku ni moja ya vifunguzi, anatakiwa kuambiwa kwamba funga yake ni sahihi. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”[3]

Hii ni kutoka kwenye Qur-aan.

Kutoka katika Sunnah ni Hadiyth ya Asmaa´ bint Abiy Bakr (Radhiya Allaahu ´anhaa) iliopokelewa na al-Bukhaariy katika ”as-Swahiyh” yake ambapo amesimulia:

“Siku moja ya mawingu wakati wa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tulifuturu. Kisha baadaye jua likachomoza.”[4]

Walikata funga yao kipindi cha mchana lakini hawakujua bali walifikiri kuwa jua limekwishazama. Jengine ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwaamrisha kulipa. Ingelikuwa kulipa ni lazima basi angeliwaamrisha. Endapo angewaamrisha basi tungenakiliwa. Lakini endapo watakata swawm kwa kufikiri kuwwa jua limekwishazama na ikabaini kuwa halijazama, basi italazimika kujizuia mpaka kuzame jua na swawm ya funga hiyo itakuwa ni sahihi.

Sharti ya pili ni kwamba anatakiwa awe mwenye kukumbuka ambayo kinyume chake ni kusahau. Endapo mfungaji atakula na kunywa kwa kusahau basi swawm yake ni sahihi. Amesema (Ta´ala):

رَبَّنَا لَا تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا

“Ee Mola wetu! Usituchukulie pale tutaposahau au tukikosea.”

Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yule mwenye kusahau ilihali amefunga ambapo akala na akanywa basi funga yake ni sahihi. Hakika si vyenginevyo Allaah ndiye kamlisha na kumnywesha.”[5]

Sharti ya tatu matakwa. Iwapo mfungaji atafanya moja katika vifunguzi hivi pasi na utashi na matakwa yake, basi funga yake ni sahihi. Kwa mfano akisukutua na maji yakateremka tumboni mwake bila matakwa yake, basi funga yake ni sahihi. Mfano mwingine mwanamme akimlazimisha mke wake kufanya jimaa na mke akashindwa kumzuia, basi funga yake ni sahihi. Kwa sababu imetokea pasi na kutaka kwake. Dalili ya hilo ni maneno Yake (Ta´ala) juu ya ambaye amekufuru pasi na kutaka kwake:

مَن كَفَرَ بِاللَّـهِ مِن بَعْدِ إِيمَانِهِ إِلَّا مَنْ أُكْرِهَ وَقَلْبُهُ مُطْمَئِنٌّ بِالْإِيمَانِ

“Atakayemkufuru Allaah baada ya kuamini kwake – isipokuwa yule aliyetenzwa nguvu na huku moyo wake umetua juu ya imani.”[6]

Mfungaji akilazimishwa kufungua au akafanya moja ya vifunguzi pasi na kutaka kwake, basi hapati dhambi yoyote na funga yake ni sahihi.

[1] 02:187

[2] Abu Daawuud (2367).

[3] 02:286

[4] al-Bukhaariy (1959).

[5] Muslim (2686).

[6] 16:106

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: 48 mas-alatu fiy Swiyaam, uk. 8-10
  • Imechapishwa: 10/04/2021