1- Alikuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) pindi anapotaka kuswali, swalah ya faradhi na ya sunnah, akielekea Ka´bah[1]. Ameamrisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na amesema kumwambia yule mtu aliyeswali vibaya:

“Unaposimama kwa ajili ya swalah, tawadha vizuri kisha uelekee Qiblah na ulete Takbiyr.”[2]

Vilevile imekuja:

“Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokuwa katika safari zake akiswali swalah za sunnah juu ya kipando chake. Anaswali Witr juu yake kokote unapoelekea, [sawa ikiwa ni mashariki au magharibi].”[3]

Kuhusu hilo kumeteremka maneno Yake (Ta´ala):

فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ

“Basi popote mnapogeuka kuna Uso Allaah.”[4]

Vilevile:

“Wakati mwingine pindi alipokuwa anataka kuswali sunnah juu ya ngamia wake, akigeuka naye Qiblah kisha akileta Takbiyr. Halafu anaswali popote kipando chake kinapoelekea.”[5]

“Alikuwa akirukuu na akisujudu juu ya kipando chake, akiashiria kwa kichwa chake na akifanya Sujuud ni yenye kushuka chini zaidi kuliko Rukuu´.”[6]

“Alikuwa anapotaka kuswali swalah ya faradhi, akishuka na akielekea Qiblah.”[7]

Ama katika khofu kubwa, amesunisha (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa Ummah wake kuswali [ifuatavyo]:

“Kwa kutembea kwa miguu au kwa kukaa juu kipando, kwa kuelekea Qiblah au kwa kutoelekea Qiblah.”[8]

Vilevile amesema:

“Wakichanganyika, kuna Takbiyr peke yake na kuashiria kwa kichwa.”[9]

Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema:

“Baina ya mashariki na magharibi ndiko kuna Qiblah.”[10]

Jaabir (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tulikuwa pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika msafara au kikosi cha jeshi. Tamahaki kukawa mawingu na tukachanganyikiwa na kutofautiana ni wapi Qiblah kipo. Matokeo yake kila mmoja akaswali kwa kuelekea upande wake. Kila mmoja wetu akachora msitari mbele yake ili kujua pahali pake. Kulipopambazuka tukaangalia na kuona kuwa tumeswali kinyume na Qiblah. Tukamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), [lakini hakutuamrisha kurudi kuswali tena] na akasema: “Swalah yenu imelipwa.”[11]

“Alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akiswali kwa kuelekea Jerusalemu [na Ka´bah ikiwa mbele yake] kabla ya kuteremshwa Aayah hii:

قَدْ نَرَىٰ تَقَلُّبَ وَجْهِكَ فِي السَّمَاءِ ۖ فَلَنُوَلِّيَنَّكَ قِبْلَةً تَرْضَاهَا ۚ فَوَلِّ وَجْهَكَ شَطْرَ الْمَسْجِدِ الْحَرَامِۚ

“Hakika Tumeona unavyogeuzageuza uso wako mbinguni. Basi Tutakuelekeza Qiblah unachokiridhia. Hivyo basi, uelekeze uso wako upande wa al-Masjid al-Haraam.”[12]

Ilipoteremshwa, akaelekea Ka´bah. Wakati watu walipokuwa wakiswali swalah ya asubuhi Qubaa´, akaja mtu na kuwaambia: “Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameteremshiwa Qur-aan usiku na ameamrishwa kuelekea Ka´bah. Hivyo ielekeeni!” Walikuwa wameelekea Shaam pindi walipogeuka [na imamu akageuka kuelekea Qiblah pamoja nao].[13]

[1] Hili ni jambo lisilokuwa na shaka yoyote kutokana na kwamba limepokelewa kwa mapokezi mengi. Kwa ajili hiyo hakuna haja ya kutaja ni wapi limepokelewa na huko mbeleni kutakuja yenye kuashiria hayo.

[2] al-Bukhaariy, Muslim och as-Siraaj.

[3] al-Irwaa’ (289) na (588).

[4] 02:115

[5] Abuu Daawuud, Ibn Hibbaan katika ”ath-Thiqaat” (1/12) na adh-Dhiyaa’ katika ”al-Mukhtaarah” ikiwa na isnadi nzuri. Ni Swahiyh kwa mujibu wa Ibn-us-Sakan, Ibn-ul-Mulaqqin katika ”Khulaaswah al-Badr al-Muniyr” (1/22) na kabla yake ´Abdul-Haqq al-Ishbiyliy katika ”al-Ahkaam” ((1394) kwa ukaguzi wangu). Haya pia ndio maoni ya Ahmad, ambayo Ibn Haani’ ameyapokea kutoka kwake katika ”al-Masaa’il” yake (1/67) katika toleo la al-Maktab al-Islaamiy.

[6] Ahmad na at-Tirmidhiy na ameisahihisha.

[7] al-Bukhaariy och Ahmad.

[8] al-Bukhaariy na Muslim.

[9] al-Bayhaqiy kwa isnadi ya al-Bukhaariy na Muslim.

[10] at-Tirmidhiy na al-Haakim na wameisahihisha. Nimeitaja katika ”Irwaa’-ul-Ghaliyl fiy Takhriyj Ahaadiyth Manaar-is-Sabiyl” (292) na Allaah amesahilisha uchapisho wake.

[11] ad-Daaraqutwniy, al-Haakim, al-Bayhaqiy, at-Tirmidhiy, Ibn Maajah na at-Twabaraaniy na imetajwa katka ”al-Irwaa’” (296).

[12] 02:144

[13] al-Bukhaariy, Muslim, Ahmad, as-Siraaj, at-Twabaraaniy (3/108/2) na Ibn Sa´d (1/243) ipo pia kwenye al-Irwaa’” (290).

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Swifatu Swalaat-in-Nabiy, uk. 75-77
  • Imechapishwa: 08/10/2016