01. Kitendo kinachomwingiza mtu Peponi

1 – Ghundur ametuhadithia, kutoka kwa Shu´bah, kutoka kwa al-Hakam: Nimemsikia´Urwah bin an-Nazzaal akihadithia kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal:

”Tulisafiri pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kutoka katika vita vya Tabuuk, nilipokuwa mwenyewe nilimuuliza: ”Ee Mtume wa Allaah! Nieleze kuhusu kitendo kitachoniingiza Peponi?” Akasema: ”Bakh! Umeulizia jambo kubwa, lakini ni jepesi kwa ambaye Allaah amemfanyia wepesi; simamisha swalah zilizofaradhishwa, kutoa zakaah iliyofaradhishwa na ukutane na Allaah hali ya kutomshirisha na chochote. Je, nisikujuze juu ya jambo muhimu kabisa, nguzo yake na nundu yake? Jambo muhimu kabisa ni Uislamu, nguzo yake ni swalah na nundu yake ni kupambana jihaad katika njia ya Allaah.”[1]

2 – ´Abiydah bin Humayd ametuhadithia, kutoka kwa al-A´mash, kutoka kwa al-Hakam, kutoka kwa Maymuun bin Abiy Shabiyb, kutoka kwa Mu´aadh ambaye amesema:

”Tulitoka pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika vita vya Tabuuk… ”

Kisha akataja Hadiyth kama hiyo.

3 – Abul-Ahwas ametuhadithia, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Rib´iy, kutoka kwa bwana mmoja katika Banu Asad, kutoka kwa ´Aliy aliyesimulia kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mtu hatohisi ladha ya imani mpaka aamini mambo manne: hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah mmoja, kwamba mimi ni Mtume wa Allaah aliyenitumiliza kwa haki, kwamba atakufa kisha atafufuliwa baada ya kufa na aamini makadirio yote.”[2]

[1] Hadiyth ni Swahiyh kupitia inayokuja baada yake. Wapokezi wake wote ni wanamme wa al-Bukhaariy na Muslim isipokuwa ´Urwah bin an-Nazzaal. Ibn Hibbaan peke yake ndiye amesema kuwa ´Urwah bin an-Nazzaal ni mwaminifu.  at-Tirmidhiy ameipokea kupitia kwa Abu Waail, kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal, na akasema:

”Hadiyth ni nzuri na Swahiyh.”

[2] Wapokezi wake wote ni waaminifu – isipokuwa Banu Asad ambaye hajulikani. Ibn Hibbaan ameipokea katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Sufyaan, kutoka kwa Mansuur, kutoka kwa Rib´iy, kutoka kwa ´Aliy – bi maana pasi na bwana huyo. at-Tirmidhiy ameipokea kupitia njia zote mbili na akaipa nguvu zaidi njia ya mwisho. Vivyo hivyo al-Haakim ambaye ameisahihisha na adh-Dhahabiy akaafikiana naye. 

  • Mhusika: Imaam Abu Bakr ´Abdullaah bin Muhammad bin Abiy Shaybah al-Kuufiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-ul-Iymaan, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 05/07/2023
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy