Himdi zote njema zinamstahiki Allaah, Mola wa walimwengu. Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, jamaa zake na Maswahabah zake wote.

Ama baada ya hayo;

Maamrisho yaliyothibiti katika Qur-aan na Sunnah juu ya kufuata yale aliyoweka Allaah na Mtume Wake na makatazo ya kuzua katika Bid´ah ni kitu chenye kujulikana vyema. Amesema (Ta´ala):

قُلْ إِن كُنتُمْ تُحِبُّونَ اللَّـهَ فَاتَّبِعُونِي يُحْبِبْكُمُ اللَّـهُ وَيَغْفِرْ لَكُمْ ذُنُوبَكُمْ ۗ وَاللَّـهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ

“Sema: “Mkiwa mnampenda Allaah, basi nifuateni mimi. Hivyo atakupendeni Allaah na atakusameheni dhambi zenu na Allaah ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu.”[1]

اتَّبِعُوا مَا أُنزِلَ إِلَيْكُم مِّن رَّبِّكُمْ وَلَا تَتَّبِعُوا مِن دُونِهِ أَوْلِيَاءَ ۗ قَلِيلًا مَّا تَذَكَّرُونَ

“Fuateni yale mliyoteremshiwa kutoka kwa Mola wenu na wala msifuate badala Yake walinzi wengine – ni machache mnayoyakumbuka.”[2]

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ

“Hii ndio njia Yangu iliyonyooka, hivyo basi ifuateni na wala msifuate njia zingine zikakufarikisheni na njia Yake!”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakika maneno ya kweli kabisa ni Kitabu cha Allaah na uongofu bora ni wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na mambo maovu kabisa ni yale yakuzua.”[4]

“Yeyote atakayezua kitendo kisichokuwa katika amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[5]

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichoafikiana na amri yetu, atarudishiwa mwenyewe.”[6]

Miongoni mwa jumla ya mambo ambayo watu wamezua ambayo ni katika Bid´ah ovu ni kusherehekea ukumbusho wa mazazi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika Rabiy´ al-Awwal. Kuna sura mbalimbali za kusherehekea:

1 – Kuna ambao wanayafanya kwa kukusanyika na wanasoma kisa cha mazazi yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) au kunasomwa mawaidha na mashairi katika mnasaba huu.

2 – Wengine wanatengeneza chakula, haluwa na vinginevyo na kuwapa wale waliohudhuria.

3 – Kuna wanaosherekea misikitini.

4 – Kuna wanaosherehekea majumbani.

5 – Kuna wengine hawatosheki na haya yaliyotajwa; wanaongeza juu ya mkusanyiko huu mambo ya haramu na maovu katika kuchanganyika kwa wanaume na wanawake, kucheza na kuimba, matendo ya kishirki kama kumuomba uokozi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kumwita, kumuomba nusura dhidi ya maadui na mengineyo.

Pasi na kujali ni sura ipi inayotumiwa na malengo yepi ya wafanyaji ni kitu kisichokuwa na shaka yoyote kabisa juu ya kwamba ni Bid´ah iliyoharamishwa na iliyozuliwa. Maulidi ni Bid´ah iliyozua Shiy´ah Faatwimiyyuun baada ya karne tatu bora kwa lengo la kuharibu dini ya waislamu. Mtu wa kwanza kuzua Bid´ah hii ni mfalme Mudhwaffar Abu Sa´iyd Kawkabuuriy ambaye alikuwa ni mfalme wa Irbil mwishoni mwa karne ya sita au mwanzoni mwa karne ya saba Hijriy. Haya yametajwa na wanahistoria mmojawapo akiwa ni Ibn Kathiyr, Ibn Khalkaan na wengineo.

Abu Shaamah amesema:

“Mtu wa kwanza kufanya hilo Mosul ilikuwa ni Shaykh ´Umar bin Muhammad al-Mullaa. Alikuwa ni mmoja katika watu wema anayejulikana. Baada ya hapo akaigwa na watu wa Irbil na wengineo.”

Haafidhw Ibn Kathiyr amesema katika “al-Bidaayah” wakati alipokuwa akielezea wasifu wa Abu Sa´iyd Kazkabuuriy:

“Alikuwa akifanya maulidi katika mwezi wa Rabi´ al-Awwal na akiyasherehekea sherehe kubwa …” Kisha akasema: “al-Bustiy amesema: ”Baadhi ya waliokuwemo katika karamu ya al-Mudhwaffar wamepokea katika baadhi ya maulidi kuwa alikuwa akitandaza katika karamu hiyo vichwa vya kuchoma 5.000, na kuku 10.000, vyungu 100.000 vya chakula na sahani 30 za haluwa …” Kisha akasema: “Alikuwa akiwafanyia Suufiyyah kisomo cha nyimbo kuanzia adhuhuri mpaka alfajiri, naye mwenyewe alikuwa akicheza pamoja nao.”[7]

Ibn Khalkaan amesema katika “Wafayaat al-A´yaan”:

“Pindi inapokuwa mwanzo wa Swafar wanapamba zile hema kwa mapambo ya kifakhari mazuri. Katika kila hema wanakaa makundi ya waimbaji na makundi ya waigizaji na ya wenye zana za pumbao. Hawakuacha ghorofa yoyote ya zile ghorofa (za hema) isipokuwa walipanga humo kundi. Maisha ya watu husimama katika kipindi hicho na hakubakia kwao kazi isipokuwa kutazama na kuzunguka juu ya sherehe hizo…” Kisha akasema: “Pindi inapokuwa kabla ya maulidi kwa siku mbili hutolewa ngamia, ng’ombe na kondoo kwa wingi mkubwa zaidi ya kuelezeka na huzipamba kwa mapigo ya ngoma, nyimbo na ala za pumbao mpaka huzileta uwanjani…” Kisha akasema: “Inapokuwa usiku wa maulidi hufanya nyimbo baada ya kuswali Maghrib katika ngome.”[8]

Hiki ndio chanzo cha kuzuka na kufufuliwa kwa sherehe za kumbukumbu ya maulidi. Yalitokea kwa kuchelewa na yakaambatana na uchezaji, upotevu na uharibifu wa mali na wakati kwa ajili tu ya Bid´ah ambayo Allaah hakuteremsha ushahidi wowote juu yake. Kinachotakikana kwa muislamu ni kuhuisha Sunnah na kufisha Bid´ah. Muislamu hatakiwi kukimbilia kufanya kitendo chochote mpaka kwanza ajue hukumu ya Allaah juu yake.

[1] 03:31

[2] 07:03

[3] 06:153

[4] Muslim (867).

[5] al-Bukhaariy (2697) na Muslim (1718).

[6] Muslim (1718).

[7] al-Bidaayah wan-Nihaayah (13/137).

[8] Wafiyaat-ul-A´yaam (03/274).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Huquwq-un-Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa sallam) bayn al-Ijlaal wal-Ikhlaal, uk. 139
  • Imechapishwa: 06/09/2025