Kwa jina la Allaah, Mwingi wa rehema, Mwenye kurehemu

Himdi zote njema ni stahiki ya Allaah.  Tunamhimidi Yeye, tunamtaka msaada, msamaha na kutubia Kwake. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpotosha, na yule aliyepotoshwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mwabudiwa wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa yupekee hana mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na Mtume Wake. Allaah (Ta´ala) amemtumiliza kwa uongofu na dini ya haki ili ishinde dini zote. Akafikisha ujumbe, akatekeleza amana na akaunasihi Ummah. Aidha akapambana kwa ajili ya Allaah ukweli wa kupambana. Akaucha Ummah wake katika njia ya wazi ambayo mchana wake ni kama usiku wake hakuna anayepotea kuiacha isipokuwa anayestahiki kuangamia – swalah na amani ziwe juu yake, kizazi chake, Maswahabah zake na wale watakaomfuata kwa wema mpaka siku ya Malipo. Namwomba Allaah anijaalie mimi na nyinyi kuwa miongoni mwa wafuasi wake kwa ndani na kwa nje, atufishe juu ya dini yake, atukusanye katika kundi lake, atuingize kwenye maombezi yake na atukusanye katika Pepo Yake yenye neema pamoja na wale aliowaneemesha ambao ni Manabii, wakweli, mashahidi na waja wema.

Amma ba´d:

Enyi Ndugu! Hakika inanifurahisha kukutana na ndugu zangu waislamu hapa na maeneo mengine yote ambayo kunatarajiwa kheri na kunaenezwa dini. Allaah amechukua ahadi kutoka kwa kila yule ambaye amempa elimu kwamba awabainishie nayo watu na wala asiifiche. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَإِذْ أَخَذَ اللَّـهُ مِيثَاقَ الَّذِينَ أُوتُوا الْكِتَابَ لَتُبَيِّنُنَّهُ لِلنَّاسِ وَلَا تَكْتُمُونَهُ فَنَبَذُوهُ وَرَاءَ ظُهُورِهِمْ وَاشْتَرَوْا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا ۖ فَبِئْسَ مَا يَشْتَرُونَ

“Wakati alipochukua Allaah fungamano la wale waliopewa Kitabu [akawaambia:] “Bila shaka mtakibainisha kwa watu na wala hamtokificha. Lakini walikitupa nyuma ya migongo yao na wakakibadilisha kwa thamani ndogo. Basi ubaya ulioje kwa yale wanayoyanunua.”[1]

Agano hili ambalo amelichukua kutoka kwa watu sio hati ambayo huandikwa na hivyo watu wakaiona. Lakini ni hati ambayo inatambulika kwa yule ambaye Allaah amempa mwenye nayo elimu. Allaah akimpa mtu elimu basi hiyo ndio hati ambayo Allaah amefunga na mwanamme au mwanamke huyu. Kwa hiyo ni lazima kwa kila ambaye ana elimu kufikisha kile alichojifunza kutoka katika Shari´ah ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) katika kila mahali na katika kila mnasaba.

[1] 03:187

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Zaad Daa´iyah ila Allaah, uk. 09-10
  • Imechapishwa: 28/10/2021