00. Sababu ya kuzungumzia mada ya Shahaadah

Himdi zote njema anastahiki Allaah. Tunamuomba msaada Yeye, msamaha na kutubia Kwake. Tunajilinda kwa Allaah kutokamana na shari ya nafsi zetu na uovu wa matendo yetu. Hakika yule mwenye kuongozwa na Allaah, basi hakuna wa kumpoteza, na yule mwenye kupotezwa na Allaah, basi hakuna wa kumwongoza. Nashuhudia ya kwamba hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah, hali ya kuwa ni Mmoja asiyekuwa na mshirika, na nashuhudia ya kwamba Muhammad ni mja na ni Mtume Wake – swalah na amani zimwendee yeye, kizazi chake, Maswahabah wake na wale wote wataomfuata na wakashikamana na Sunnah zake hadi siku ya Qiyaamah.

Ama baada ya hayo;

Hakika Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ametuamrisha kumtaja na akawasifu wale wenye kumtaja na akawaahidi ujira uliokuwa mkubwa. Ametuamrisha kumtaja kwa njia isiyofungamana na vilevile baada ya kumaliza ´ibaadah mbalimbali. Amesema (Ta´ala):

فَإِذَا قَضَيْتُمُ الصَّلَاةَ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِكُمْ

“Mtakapomaliza swalah, basi mtajeni Allaah hali ya kusimama, kukaa na [mnapojinyosha] ubavuni mwenu.” (04:103)

فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا

“Mtakapomaliza kutekeleza ‘ibaadah za hajj zenu, basi mtajeni Allaah kama mnavyowataja baba zenu au mtajeni zaidi.” (02:200)

Vilevile ameamrisha kumtaja katikati ya ´ibaadah ya hajj. Amesema (Ta´ala):

فَإِذَا أَفَضْتُم مِّنْ عَرَفَاتٍ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ عِندَ الْمَشْعَرِ الْحَرَامِ

“Basi mtakapomiminika kutoka ‘Arafaat, basi mtajeni Allaah kwenye Mash’ar al-Haraam.” (02:198)

وَيَذْكُرُوا اسْمَ اللَّـهِ فِي أَيَّامٍ مَّعْلُومَاتٍ عَلَىٰ مَا رَزَقَهُم مِّن بَهِيمَةِ الْأَنْعَامِ

“Walitaje Jina la Allaah katika siku maalum juu ya wale wanyamahoa aliyowaruzuku.” (22:28)

Ameweka kusimamisha swalah kwa ajili ya kumtaja. Amesema (Ta´ala):

وَأَقِمِ الصَّلَاةَ لِذِكْرِي

“Simamisha swalah kwa ajili ya kunitaja.” (20:14)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Masiku ya kuchinja ni kwa ajili ya kula, kunywa na kumtaja Allaah.”[1]

Amesema (Ta´ala) tena:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا اذْكُرُوا اللَّـهَ ذِكْرًا كَثِيرًا وَسَبِّحُوهُ بُكْرَةً وَأَصِيلًا

“Enyi mlioamini! Mtajeni Allaah kwa kumtaja kwa wingi na msabihini asubuhi na jioni.” (33:41-42)

Ilipokuwa Dhikr bora kabisa ni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa yupekee hana mshirika`[2], kama ilivyothibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Du´aa bora ni ile ya ´Arafah na bora nilichosema mimi na Mitume wengine waliokuwa kabla yangu ni ´hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah hali ya kuwa yupekee hana mshirika. Ufalme wote ni Wake na himdi zote njema anastahiki Yeye – Naye juu ya kila kitu ni Muweza`.”[3]

Kadhalika ilipokuwa neno hili kubwa ”hapana mungu wa haki isipokuwa Allaah” lina nafasi ya juu kabisa ukilinganisha na aina mbalimbali zingine za Adhkaar na isitoshe limefungamana na hukumu, masharti, maana na yanayopelekea kwalo – kwa msemo mwingine ni kwamba sio neno linalotamkwa kwa ulimi peke yake – ndipo nikapendelea iwe maudhui ya mazungumzo yetu na huku tukitarajia kutoka kwa Allaah (Ta´ala) atujaalie sisi na nyinyi kuwa miongoni mwa watu wake ambao wanashikamana nalo, wenye kutambua maana yake, wenye kutendea yale inalopelekea kwa nje na kwa ndani.

Mazungumzo ya mada yetu itakuwa ni yenye kuzungumzia nukta zifuatazo:

1 – Nafasi ya shahaadah katika maisha.

2 – Fadhilah zake.

3 – Uchambuzi wake wa kisarufi.

4 – Nguzo zake.

5 – Sharti zake.

6 – Maana yake.

7 – Yanayopelekea kwalo.

8 – Lini linamfaa yule mwenye kulitamka na lini halimfai.

9 – Athari yake.

Nasema yafuatayo hali ya kuwa ni mwenye kumtaka msaada Allaah:

[1] Muslim (1141) na Ahmad (05/75).

[2] Laa ilaaha illa Allaah wahdahuu laa shariyka lahuu.

[3] at-Tirmidhiy (3585).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ma´naa laa ilaaha illa Allaah, uk. 8-9
  • Imechapishwa: 22/09/2023