Allaah (´Azza wa Jall) amesema:

وَإِذَا قِيلَ لَهُمْ لَا تُفْسِدُوا فِي الْأَرْضِ قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَـٰكِن لَّا يَشْعُرُونَ

“Wanapoambiwa “Msifanye ufisadi katika ardhi” basi husema “Hakika sisi ni watengenezaji.” Zindukeni! Hakika wao ndio waharibifu lakini hawahisi.”[1]

Pindi wanafiki hawa wanapokatazwa kueneza uharibifu ardhini, nao ni ule ukafiri, maasi, kutoa siri za waumini kwa adui zao na kujenga urafiki na makafiri, husema:

و قَالُوا إِنَّمَا نَحْنُ مُصْلِحُونَ

“Husema “Hakika sisi ni watengenezaji.”

Wakakusanya kati ya kueneza ufisadi ardhini na kudhihirisha kuwa sio ufisadi na bali ni kutengeneza, jambo ambalo ni kupindua uhakika wa mambo. Wamekusanya kati ya kitendo cha batili na kuonelea kuwa ni haki. Hili ndio janga kubwa kwa yule mwenye kutenda maasi. Ambaye yuko karibu kidogo na usalama na kuna matarajio kwake ya kujirejea ni yule anayetambua kuwa ni maasi.

أَلَا إِنَّهُمْ هُمُ الْمُفْسِدُونَ وَلَـٰكِن لَّا يَشْعُرُونَ

“Zindukeni! Hakika wao ndio waharibifu lakini hawahisi.”

Hakika hakuna uharibifu mkubwa kuliko yule ambaye amezikufuru Aayah za Allaah, akazuia kutokamana na njia ya Allaah, akamdanganya Allaah na mawalii Wake, kujenga urafiki na wale wanaompiga vita Allaah na Mtume Wake. Pamoja na haya yote wanadai kuwa ni kutengeneza. Je, kuna ufisadi mkubwa wenye kushinda huu? Lakini hawajui elimu yenye kuwanufaisha ingawa wanaweza kuwa wanajua ujuzi ambao ni hoja dhidi yao mbele ya Allaah.

[1] 02:11-12

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, sid. 32
  • Imechapishwa: 07/05/2020