Waislamu kujipinda katika nyusiku kumi za mwisho

Swali: Kwa mnasaba wa usiku wa Qadr tunapenda kutoka kwa muheshimiwa kuwazungumzia waislamu wote juu ya mnasaba huu mtukufu.

Jibu: Usiku wa Qadr ndio usiku bora. Allaah (Ta´ala) ameteremsha ndani yake Qur-aan na akakhabarisha kwamba ni bora kuliko miezi elfu, kwamba ni wenye baraka na kwamba katika usiku huo kunapambanuliwa kila jambo lenye hekima. Amesema (Subhaanah):

حم وَالْكِتَابِ الْمُبِينِ إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةٍ مُّبَارَكَةٍ ۚ إِنَّا كُنَّا مُنذِرِينَ فِيهَا يُفْرَقُ كُلُّ أَمْرٍ حَكِيمٍ

“Haa Miym. Naapa kwa Kitabu kinachobainisha. Hakika Sisi tumeiteremsha katika usiku uliobarikiwa, hakika Sisi daima ni Wenye kuonya. Katika [usiku] huo hupambanuliwa kila jambo la hekima.”[1]

إِنَّا أَنزَلْنَاهُ فِي لَيْلَةِ الْقَدْرِ وَمَا أَدْرَاكَ مَا لَيْلَةُ الْقَدْرِ  لَيْلَةُ الْقَدْرِ خَيْرٌ مِّنْ أَلْفِ شَهْرٍتَنَزَّلُ الْمَلَائِكَةُ وَالرُّوحُ فِيهَا بِإِذْنِ رَبِّهِم مِّن كُلِّ أَمْرٍ سَلَامٌ هِيَ حَتَّىٰ مَطْلَعِ الْفَجْرِ

“Hakika Sisi tumeiteremsha Qur-aan katika usiku wa Qadr. Na kipi kitakachokujulisha ni nini huo usiku wa Qadr? Usiku wa Qadr ni mbora kuliko miezi elfu: wanateremka humo Malaika na Roho kwa idhini ya Mola wao kwa kila jambo. Ni amani mpaka kuchomoza alfajiri!”[2]

Pia imesihi kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Yule atakayesimama kuswali usiku wa Qadr kwa imani na kwa matarajio, basi atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia.”

Kuusimamisha kunakuwa kwa kuswali, kuleta Adhkaar, kuomba du´aa, kusoma Qur-aan na matendo mbalimbali ya kheri.

Suurah hii imejulisha kuwa matendo katika usiku huo ni bora kuliko matendo ya miezi elfu tukiondoa usiku huo. Hii ni fadhilah tukufu na rehema kutoka kwa Allaah kwenda kwa waja Wake. Kwa hiyo waislamu wana kila haki ya kuuadhimisha na kuuhuisha kwa kufanya ´ibaadah.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameeleza kuwa usiku wa Qadr unakuwa katika zile siku kumi za mwisho za Ramadhaan na kwamba zile nyusiku za witiri ni zenye nguvu zaidi kuliko nyusiku nyenginezo. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Utafuteni katika zile nyusiku kumi za mwisho za Ramadhaan na utafuteni katika kila usiku wa witiri.”

Hadiyth Swahiyh zilizopokelewa kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zimejulisha kwamba usiku wa Qadr ni wenye kuhamahama ndani ya nyusiku kumi hizi na hauwi siku zote kwenye usiku mmoja. Usiku wa Qadr unaweza kuwa katika usiku wa tarehe ishirini na moja, usiku wa tarehe ishini na tatu, usiku wa tarehe ishirini na tano, usiku wa tarehe ishirini na saba – na ndio usiku wenye nguvu zaidi – na unaweza kutokea katika usiku wa tarehe ishirini na tisa na pia vivyo hivyo unaweza kujitokeza katika zile nyusiku za shufwa. Yule ambaye atasimama kuswali nyusiku zote kwa imani na kwa matarajio basi ataupata usiku huu pasi na shaka yoyote na atafuzu kwa yale ambayo Allaah amewaahidi wenye nao.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akizifanya maalum nyusiku hizi kwa kujipinda zaidi kiasi ambacho hakifanyi katika zile ishirini za mwanzo. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akijitahidi katika zile nyusiku za mwisho za Ramadhaan kuliko anavyojitahidi katika nyusiku zengine.”

Pia amesema:

“Mtume  (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa zinapoingia zile siku kumi za mwisho basi anahuisha usiku, anaiamsha familia yake, anakuwa jadi na hufunga vizuri kikoi chake.”[3]

Mara nyingi alikuwa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifanya I´tikaaf ndani ya nyusiku hizi. Allaah (Ta´ala) amesema:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ

“Hakika mna kigezo kizuri kwa Mtume wa Allaah.”[4]

´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) alimuuliza:

“Ee Mtume wa Allaah! Nikikutana na usiku wa Qadr niseme nini ndani yake?” Akasema: “Sema:

اللَّهُمَّ إِنَّكَ عُفُوٌّ تُحِبُّ الْعَفْوَ فَاعْفُ عَنِّي

“Ee Allaah! Hakika Wewe ni Mwingi wa kusamehe na unapenda kusamehe. Hivyo basi, nisamehe.”[5]

Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allahu ´anhum) na Salaf waliokuja baada yao walikuwa wakiadhimisha nyusiku hizi kumi na wakijipinda ndani yake kwa kufanya kheri mbalimbali.

Jambo lililosuniwa kwa waislamu kila mahali wamuige Mtume wao (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), Maswahabah zao watukufu (Radhiya Allaahu ´anhum) na Salaf wema wa Ummah huu kwa njia ya wao kuhuisha nyusiku hizi kwa kuswali, kusoma Qur-aan na aina mbalimbali za Adhkaar na ´ibaadah. Wayafanye hayo yote kwa imani na kwa matarajio ili wafuzu kusamehewa kwa madhambi, kufutiwa madhambi na kuachwa huru na Moto – ikiwa ni fadhilah na ukarimu kutoka Kwake (Subhaanah).

[1] 44:01-04

[2] 97:01-05

[3] al-Bukhaariy (2024) na Muslim (1174).

[4] 33:31

[5] Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh Sunan at-Tirmidhiy” (3513).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (15/425)
  • Imechapishwa: 16/05/2020