Uharamu wa kutumia hariri na vyombo vya dhahabu na fedha

384- Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuvaa hariri hapa duniani basi hatoivaa huko Aakhirah. Yule mwenye kunywa pombe hapa duniani basi hatoinywa huko Aakhirah. Yule mwenye kunywa ndani ya chombo cha dhahabu na cha fedha, basi hatokunywa ndani yavyo huko Aakhirah.” Halafu akasema: “Mavazi ya watu wa Peponi, kinywaji cha watu wa Peponi na vyombo vya watu wa Peponi.”

Ameipokea al-Haakim (4/141) na Ibn ´Asaakir katika ”Taariykh Dimashq” (2/202/15) kupitia kwa Yahyaa bin Hamzah: Zayd bin Waaqid amenihadithia: Khaalid bin ´Abdillaah bin Husayn amemuhadithia: Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amenihadithia kwamba Mtume wa Allaah Allâhs sändebud (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema…

Akasema:

“Cheni ya wapokezi wake ni Swahiyh.”

adh-Dhahabiy ameafikiana naye.

Tambua kwamba Hadiyth zinazoharamisha kuvaa hariri, kunywa pombe na kunywa ndani ya vyombo vya dhahabu na vya fedha ni nyingi sana kiasi cha kwamba haziwezi kudhibitiwa. Nimependa kuitaja hii kwa sababu imekusanya maneno juu ya vitu hivi vitatu na kwa mtiririko mmoja. Kisha akamalizia kwa kusema: “Mavazi ya watu wa Peponi, kinywaji cha watu wa Peponi na vyombo vya watu wa Peponi.”

Allaah ameharamisha mavazi ya hariri kwa wanamme peke yao. Kwa sababu ndio yatakuwa mavazi yao Peponi. Amesema (Ta´ala):

وَلِبَاسُهُمْ فِيهَا حَرِيرٌ

“Mavazi yao humo ni hariri.”[1]

Akaharamisha pombe kwa wanamme na wanawake kwa sababu ni kinywaji chao huko Peponi:

مَّثَلُ الْجَنَّةِ الَّتِي وُعِدَ الْمُتَّقُونَ ۖ فِيهَا أَنْهَارٌ مِّن مَّاءٍ غَيْرِ آسِنٍ وَأَنْهَارٌ مِّن لَّبَنٍ لَّمْ يَتَغَيَّرْ طَعْمُهُ وَأَنْهَارٌ مِّنْ خَمْرٍ لَّذَّةٍ لِّلشَّارِبِينَ وَأَنْهَارٌ مِّنْ عَسَلٍ مُّصَفًّى ۖ وَلَهُمْ فِيهَا مِن كُلِّ الثَّمَرَاتِ وَمَغْفِرَةٌ مِّن رَّبِّهِمْ

“Mfano wa Pepo ambayo wameahidiwa wenye kumcha Allaah ndani yake mna mito ya maji yasiyovunda na mito ya maziwa haitabadilika ladha yake na mito ya mvinyo yenye ladha kwa wanywaji na mito ya asali iliyosafishwa. Aidha watapata humo kila aina ya matunda na msamaha kutoka kwa Mola wao.”[2]

Akaharamisha kunywa ndani ya vyombo vya dhahabu na vya fedha kwa wanamme na kwa wanawake pia kwa sababu vyombo vyao:

ادْخُلُوا الْجَنَّةَ أَنتُمْ وَأَزْوَاجُكُمْ تُحْبَرُونَ يُطَافُ عَلَيْهِم بِصِحَافٍ مِّن ذَهَبٍ وَأَكْوَابٍ

”Ingieni Peponi nyinyi na wake zenu mfurahishwe. Watapitishiwa sahani za dhahabu na vikombe.”[3]

Yule mwenye kuharakisha kujiburudisha navyo pasi na kuwa mwenye kujali wala mwenye kutubia basi ataadhibiwa kwa kunyimwa navyo huko Aakhirah. Kitendo ni sawa na malipo.

[1] 35:33

[2] 47:15

[3] 43:70-71

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (1/2/738-739)
  • Imechapishwa: 29/05/2021