Sisi tunalingania katika Qur-aan na Sunnah kwa mfumo wa Salaf. Nakujengea dhana nzuri na kusema kwamba unakubaliana nami katika haya, lakini inadhihiri kuwa hukubaliani nasi kutokana na sababu moja au nyingine.

Umefikwa na yaleyale yaliyowafika watu wengi hii leo. Usichukulie vibaya. Msimamo wako huu ni lazima uwekewe wazi na dini ni kupeana nasaha. Leo wako watu ambao wanafanya inda na wanaenda kinyume na maneno ya Salaf na ya maimamu na wakajulisha kitu kisichojulikana kwa wanazuoni, nacho ni kile kinachoitwa hii leo uasi dhidi ya watawala.

Tunaona kuwa baadhi ya uasi unafaa na mwingine haufai, kama ilivyotajwa wazi katika Sunnah[1].

[1] Imaam Ibn ´Uthaymiyn (Rahimahullaah) amesema:

”Muslim amepokea kupitia kwa Umm Salamah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtakuwa na viongozi ambao mtayajua mambo fulani na mengine mtayapinga. Yule mwenye kuchukia ametakasika na mwenye kukemea amesalimika. Tatizo liko kwa yule mwenye kuridhia na kufuata.” Wakasema: “Ee Mtume wa Allaah! Je, tusiwapige vita?” Akasema: “Hapana, maadamu wanaswali.”

Amepokea tena kupitia kwa ´Awf bin Maalik (Radhiya Allaahu ´anh) aliyesimulia ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Viongozi wenu bora kabisa ni wale mnaowapenda nao wanakupendeni na wale mnaowaombea nao wanakuombeeni. Viongozi wenu waovu kabisa ni wale mnaowachukia nao wanakuchukieni na mnawalaani nao wanakulaanini.” Kukasemwa: Ee Mtume wa Allaah! Tusiwaondoshe kwa panga?” Akasema: “Hapana, midhali wanasimamisha swalah kati yenu. Mkiona kitu mnachokichukia kutoka kwa mtawala wenu, chukieni kitendo chake bila ya kunyanyua mkono kutoka katika utiifu.”

Hadiyth hizi mbili zilizotajwa zinafahamisha kuwa mtawala anatakiwa kupigwa vita endapo hatosimamisha swalah. Haijuzu kupambana na kuwapiga vita watawala isipokuwa pale watapofanya kufuru ya wazi kabisa ambayo tuko na dalili kutoka kwa Allaah (Ta´ala). ´Ubaadah bin as-Swaamit (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituita na tukampa kiapo cha usikivu na utiifu juu ya kusikiza na kutii katika yale tunayoyapenda na kuyachukia, katika kipindi kichepesi na kizito, pindi mtu anapotangulizwa juu yetu na tusizozane na mtawala maadamu hamjaona kufuru ya wazi ambayo mko na dalili kwayo kutoka kwa Allaah.”

Inafahamisha kuwa mtawala kuacha kwake swalah, ambako Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekufungamanisha na kuwafanyia uasi, ni dalili kutoka kwa Allaah juu ya ukafiri wao wa wazi.” (Hukm Taarik-is-Swalaah, uk. 7-8)

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (877) Dakika: 15:08
  • Imechapishwa: 03/07/2021
  • taaliki: Firqatunnajia.com