Tawbah ya mwenye kuritadi kutoka katika Uislamu


Swali: Mwenye kufanya moja katika vitenguzi vya Uislamu halafu akatubia baada ya hapo. Je, tawbah yake inakubaliwa?

Jibu: Ndio. Akitubu basi Allaah anamsamehe. Allaah anaikubali tawbah kutoka kwa watenda madhambi wote. Ni mamoja wakawa walioritadi au wengineo. Amesema (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَإِنِّي لَغَفَّارٌ لِّمَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا ثُمَّ اهْتَدَىٰ

“Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe kwa anayetubia na akaamini na akatenda mema kisha akanyooka barabara.”[1]

قُلْ يَا عِبَادِيَ الَّذِينَ أَسْرَفُوا عَلَىٰ أَنفُسِهِمْ لَا تَقْنَطُوا مِن رَّحْمَةِ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ يَغْفِرُ الذُّنُوبَ جَمِيعًا

“Sema: Enyi waja Wangu ambao wamechupa mipaka juu ya nafsi zao: “Msikate tamaa na rehema za Allaah, hakika Allaah anasamehe dhambi zote.”[2]

إِنَّ الَّذِينَ كَفَرُوا بَعْدَ إِيمَانِهِمْ ثُمَّ ازْدَادُوا كُفْرًا لَّن تُقْبَلَ تَوْبَتُهُمْ

”Hakika wale waliokufuru baada ya kuamini kwao halafu wakazidi kukufuru, haitokubaliwa tawbah yao.”[3]

وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ

”Atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, akafariki hali ya kuwa ni kafiri… ”[4]

Bi maana yule mwenye kuritadi na asitubie mpaka akafa huyu amezidisha ukafiri kwa vile ameendelea juu ya ukafiri. Lakini iwapo angelitubia kabla ya kufa basi Allaah angemsamehe. Maneno Yake (Subhaanah):

وَمَن يَرْتَدِدْ مِنكُمْ عَن دِينِهِ فَيَمُتْ وَهُوَ كَافِرٌ فَأُولَـٰئِكَ حَبِطَتْ أَعْمَالُهُمْ فِي الدُّنْيَا وَالْآخِرَةِ ۖ وَأُولَـٰئِكَ أَصْحَابُ النَّارِۖ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ

“Atakayeritadi miongoni mwenu kutoka dini yake, akafariki hali ya kuwa ni kafiri, basi hao yameporomoka matendo yao duniani na Aakhira – na hao ni watu wa Motoni wao humo ni wenye kudumu.”

ni dalili inayofahamisha kwamba iwapo akifa ilihali ni muislamu aliyetubia, Allaah anamsamehe. Kwa sababu Allaah anaikubali tawbah kutoka kwa murtadi na mwengine pindi atapotubia kwa Allaah (´Azza wa Jall).

[1] 20:82

[2] 39:53

[3] 03:90

[4] 02:217

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 31-32
  • Imechapishwa: 03/03/2019