Ni lini mtu anazingatiwa amewahi swalah ya mkusanyiko?


Swali: Ambaye amemuwahi imamu katika Tashahhud ya mwisho anazingatiwa ameiwahi swalah ya mkusanyiko na fadhilah zake?

Jibu: Baadhi ya wanachuoni katika Hanaabilah na wengineo wamesema kwamba akileta Takbiyrat-ul-Ihraam na akaketi chini kabla ya imamu kutoa Tasliym, basi ameiwahi swalah ya mkusanyiko. Kikosi cha wanachuoni wengine wamesema kuwa hawahi swalah ya mkusanyiko isipokuwa kwa kuwahi Rak´ah moja, maoni ambayo ndio ya sawa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuwahi Rak´ah moja pamoja na imamu basi amewahi [swalah ya] mkusanyiko.”

Kwa hivyo swalah ya mkusanyiko haiwahiwi isipokuwa kwa kuwahi Rak´ah moja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule mwenye kuwahi Rak´ah moja ya ´Aswr kabla ya jua kuzama, basi ameiwahi ´Aswr. Na yule mwenye kuwahi Rak´ah moja ya Subh kabla ya jua kuchomoza, basi ameiwahi Subh.”

Kwa hivyo wakati wa swalah unawahiwa kwa kuwahi Rak´ah moja. Vivyo hivyo swalah ya mkusanyiko inawahiwa kwa kuwahi Rak´ah moja. Haya ndio maoni ya sawa.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (19)
  • Imechapishwa: 01/02/2021