Namna ya kutangamana na makafiri katika krismasi

Swali: Ni ipi hukumu ya kuwapongeza makafiri kwa sikukuu ya krismasi? Ni vipi tuwajibu wao wakitupongeza? Je, inajuzu kwenda zile sehemu za sherehe zao ambapo wanafanya minasaba hii? Je, mtu anapata dhambi akifanya kitu katika hayo yaliyotajwa pasi na kukusudia bali amefanya hivo ima kwa sababu ya kuwapaka mafuta, kuona haya, kuona uzito au sababu nyenginezo? Je, inafaa kujifananisha nao katika jambo hilo?

Jibu: Kuwapongeza makafiri kwa sikukuu ya krismasi au kwa sikukuu nyenginezo za kidini ni kitendo cha haramu kwa maafikiano. Hayo yamenukuliwa na Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika kitabu chake “Ahkaam Ahl-idh-Dhimmah” ambapo amesema:

“Kuwapongeza kwa nembo za kikafiri ambazo ni maalum kwao ni jambo la haramu kwa maafikiano. Kwa mfano kuwapongeza kwa sikukuu zao na funga zao kwa kusema: “Nakutakia sikukuu yenye furaha” au “Nakupongeza kwa sikukuu hii” na mfano wake. Kitendo hichi, mwenye nacho akisalimika na ukafiri basi ni miongoni mwa mambo ya haramu. Ni jambo ambalo liko katika kiwango cha kuwapongeza kwa kusujudia kwake msalaba. Bali kitendo hicho [cha pongezi] ni dhambi kubwa mbele ya Allaah na cha hasira zaidi mbele Yake kuliko kumpongeza kwa kunywa pombe, kuiua nafsi, kuizini tupu ya haramu na mfano wake. Watu wengi ambao hawajui hadhi ya dini wanatumbukia katika jambo hilo ilihali hawajui ubaya wa walichokifanya. Anayempongeza mja kwa maasi, uzushi au ukafiri basi amejipelekea mwenyewe katika hasira na ghadhabu za Allaah”.

Kuwapongeza makafiri kwa ajili ya sikukuu zao ni jambo la haramu kwa sababu hizi zilizotajwa na Ibn-ul-Qayyim. Kwa sababu ndani yake kuna kuwasapoti katika yale wanayoyafanya katika nembo za kikafiri na kuwaridhia ingawa yeye haridhii ukafiri huu kwa dhati yake. Lakini hata hivyo ni haramu kwa muislamu kuridhia nembo za ukafiri au kumpongeza mwengine kwazo. Kwa sababu Allaah (Ta´ala) haridhii jambo hilo. Allaah (Ta´ala) amesema:

إِن تَكْفُرُوا فَإِنَّ اللَّـهَ غَنِيٌّ عَنكُمْ ۖ وَلَا يَرْضَىٰ لِعِبَادِهِ الْكُفْرَ ۖ وَإِن تَشْكُرُوا يَرْضَهُ لَكُمْ

“Mkikufuru, basi hakika Allaah ni mkwasi kwenu, na wala haridhii kwa waja Wake ukafiri na mkishukuru huridhika nanyi.” (39:07)

الْيَوْمَ أَكْمَلْتُ لَكُمْ دِينَكُمْ وَأَتْمَمْتُ عَلَيْكُمْ نِعْمَتِي وَرَضِيتُ لَكُمُ الْإِسْلَامَ دِينًا

 “Leo wamekata tamaa wale waliokufuru juu ya dini yenu, hivyo basi msiwaogope na niogopeni Mimi. Leo nimekukamilishieni dini yenu na nimekutimizieni neema Yangu na nimekuridhieni Uislamu uwe dini yenu.” (05:03)

Kuwapongeza kwazo ni kitendo cha haramu. Ni mamoja mtu anashirikiana naye kazini au hapana.

Wao wakitupongeza kwa sikukuu zao hatuwaitikii juu ya jambo hilo. Kwa sababu sio sikukuu zetu. Jengine ni kwa sababu ni sikukuu zisizoridhiwa na Allaah (Ta´ala). Kwa sababu ima zimezuliwa katika dini yao au zimewekwa katika Shari´ah yao. Lakini hata hivyo baadaye zimefutwa kwa dini ya Uislamu ambayo Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ametumilizwa kwayo kwenda kwa viumbe wote. Amesema kuhusu dini hiyo:

وَمَن يَبْتَغِ غَيْرَ الْإِسْلَامِ دِينًا فَلَن يُقْبَلَ مِنْهُ وَهُوَ فِي الْآخِرَةِ مِنَ الْخَاسِرِينَ

“Yeyote anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitokubaliwa kwake naye Aakhirah atakuwa miongoni mwa waliokhasirika.” (03:85)

Muislamu kuitikia wito wao kwa mnasaba huu ni haramu. Kwa sababu kitendo hicho ni khatari zaidi kuliko yule anayewapongeza kwa sababu ya kule kushirikiana nao katika mambo hayo.

Vivyo hivyo ni haramu kwa waislamu kujifananisha na makafiri kwa kufanya sherehe kwa minasaba hii, kupeana zawadi, vitu tamtam, kupika chakula, kuacha kufanya kazi na mfano wake. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kujifananisha na watu basi yeye ni katika wao.”

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema katika kitabu chake “Iqtidhwaa´-us-Swiraatw al-Mustaqiym”:

“Kujifananisha nao katika baadhi ya sikukuu zao kunapelekea kuzifurahisha nyoyo zao kwa ile batili waliyomo. Huenda likawapa matumaini ya kutumia fursa hiyo na kuwatumia wale [waislamu] madhaifu.”

Mwenye kufanya kitu katika hayo anapata dhambi. Ni mamoja amefanya hivo kwa sababu ya kutaka kuwapaka mafuta, kuwapenda, kuona haya au kwa sababu nyingine. Kwa sababu ni katika kufanya Mudaanah[1] katika dini ya Allaah na ni miongoni mwa kuzifanya nyoyo za makafiri kuwa na nguvu na wakafurahikia dini yao.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/132-masuala-yanayohusiana-na-jinsi-ya-kutangamana-na-mzazi-kafiri/

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://ar.islamway.net/fatwa/4582/%D8%A7%D9%84%D8%AA%D9%87%D9%86%D8%A6%D8%A9-%D8%A8%D8%B9%D9%8A%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D9%83%D8%B1%D9%8A%D8%B3%D9%85%D8%A7%D8%B3
  • Imechapishwa: 17/12/2019