Mwanamke kutembea hadharani na ´Abaa´ah juu ya mabega

Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke kuswali na huku ameweka ´Abaa´ah yake juu ya mabega yake? Imenifikia kutoka kwako kwamba katika hali hii swalah yake inabatilika kwa kuwa imefanana na vazi la mwanaume.

Jibu: Allaah ndiye Mwenye kutakwa msaada. Mwanamke huyu imepokelewa vilevile kinyume chake katika yale yaliyoenezwa na wanawake kwamba sisi tunasema kwamba ni sawa kwa mwanamke kuvaa ´Abaa´ah juu ya mabega hata kama hilo litafanywa sokoni na madukani. Yote mawili ni makosa.

Sisi tunasema mwanamke kuweka ´Abaa´ah juu ya mabega yake wakati wa swalah hakuna neno. Kwa sababu hili ni jambo lililozoeleka kwa wanawake. Si jambo maalum kwa wanaume peke yao mpaka tuseme kuwa huku ni kujifananisha na wanaume.

Kuhusu mwanamke kuweka ´Abaa´ah yake juu ya mabega masokoni na mbele za watu asifanye hivo. Kwa sababu kule kuweka kwake ´Abaa´ah yake juu ya mabega kunapelekea kufichukua fomu ya mabega yake na shingo yake na kuonyesha kama shingo yake ni ndefu au ni fupi, jambo ambalo ni fitina. Iwapo wanawake wataruhusiwa kuweka ´Abaa´ah zao masokoni ni nani ambaye ana uhakika kama mambo hayatokuwa na wanawake wakaanza kutoka masokoni wakiwa na kanzu pasi na ´Abaa´ah? Kwa sababu wanawake mara nyingi wakifunguliwa mlango kidogo basi mlango unakuwa mkubwa. Huenda wakafikia mpaka kuufungua mlango wote na wakaingia kusikokuwa mlango.

Kwa hiyo tunasema kuweka ´Abaa´ah juu ya mabega wakati wa swalah hakuna neno. Hakubatilishi swalah. Ama kutembea nayo masokoni hapana. Kwa sababu kunapelekea katika fitina. Ni njia inayopelekea wanawake kupanuka zaidi katika mavazi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (42) http://binothaimeen.net/content/928
  • Imechapishwa: 25/11/2018