Muislamu aliye na msimamo anamtii mtawala wake


Swali: Tunawaona baadhi ya vijana ambao Allaah amewaongoza kushikamana na Qur-aan na Sunnah na walikuwa na hamasa yenye nguvu juu ya Da´wah. Siku miongoni mwa siku wakifikwa na fitina kama vile kutotoa kalima au Khutbah au wakakatazwa na mahakama basi utawaona namna wanavyojirudia. Bali baadhi wanafikia kuacha kuwa na msimamo katika dini.

Jibu: Sikuelewa wajihi wa swali.

Swali: Ni zipi nasaha zako?

Jibu: Miongoni mwa utimilifu wa kuwa na msimamo katika dini ni kumtii mtawala katika yale mambo yasiyokuwa maasi. Sisi hatuwatii watawala kwa sababu wanatokamana na familia fulani. Tunawatii kwa sababu Allaah ndiye ametuusia jambo hilo:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

“Enyi walioamini! Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”[1]

Tunaamini kuwa kuwatii katika yale mambo yasiyokuwa maasi ni kumtii Allaah (´Azza wa Jall). Tunawaambia watu hawa kwamba hakuna chochote kinachowalazimu:

أَطِيعُوا اللَّـهَ وَأَطِيعُوا الرَّسُولَ وَأُولِي الْأَمْرِ مِنكُمْ

Mtiini Allaah na mtiini Mtume na wenye madaraka katika nyinyi.”

Kunaingia katika kumtii Allaah. Muda wa kuwa hawakukuamrisheni kunywa pombe au chochote katika mambo ya haramu mnapaswa kuwatii.

Swali: Ni jambo linatokea mara nyingi kwamba wanafika wanajirudi kutokana na fitina kama hii.

Jibu: Hili ni tatizo. Allaah ameashiria jambo hilo ndani ya Qur-aan:

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَعْبُدُ اللَّـهَ عَلَىٰ حَرْفٍ فَإِنْ أَصَابَهُ خَيْرٌ اطْمَأَنَّ بِهِ ۖ وَإِنْ أَصَابَتْهُ فِتْنَةٌ انقَلَبَ عَلَىٰ وَجْهِهِ خَسِرَ الدُّنْيَا وَالْآخِرَةَ ۚ ذَٰلِكَ هُوَ الْخُسْرَانُ الْمُبِينُ

“Miongoni mwa watu yuko yule anayemwabudu Allaah ukingon, inapompata kheri, hupata matumaini kwayo, na anapofikwa na mitihani hugeuka nyuma juu ya uso wake; amekhasirika duniani na Aakhirah. Hiyo ndiyo khasara ya wazi.”[2]

Mche Allaah! Maadamu unajua kuwa ni lazima kumtii mtawala na amekukataza kuzungumza na unatambua kuwa ni katika dini ya Allaah, basi wewe uko katika kheri.

´Ammaar bin Yaasir alikuwa anaona kwamba mwenye janaba na akakosa maji anatakiwa kufanya Tayammum. ´Umar bin al-Khattwaab alikuwa haonelei hivo na badala yake anaona kuwa aliye na janaba anatakiwa kukaa mpaka pale ambapo atapata maji ambapo ataoga na kuswali. ´Ammaar bin Yaasir alikuwa anawafikishia watu kwamba aliye na janaba na akakosa maji basi anatakiwa kufanya Tayammum. Haya yalitokea wakati ambapo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa amemtuma yeye na ´Umar katika kazi fulani.  ´Ammaar akapatwa na janaba na akaanza kujigaragaza kwenye mchanga kama ambavo mnyama unajigaragaza kwenye mchanga. Halafu aliporudi akamweleza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) yaliyotokea. Ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamwambia: “Ilikuwa inakutosha kufanya kwa mikono yako namna hii” ambapo akapiga kwa mikono yake ardhini na akapangusa uso na mikono yake. Pindi ´Umar alipofikiwa na khabari kwamba anahadithia Hadiyth hii, basi akamwagizia mjumbe na akamuuliza ni mambo gani anayofanya. Akasema: “Ee kiongozi wa waumini! Hivi hukumbuki wakati Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotutuma mimi na wewe kwenda kufanya kazi fulani?” ´Ammaar akaendelea kusema: “Ee kiongozi wa waumini! Ukitaka nitendee kazi kwa mujibu wa amri ya Allaah na kukutii kwa njia ya kwamba nisizungumzie jambo hili, basi nitaacha kufanya hivo.” Amesema hivo juu ya Hadiyth kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). ´Umar akasema: “Hapana. Tunakuacha ufanye kile ulichokwishakianza.” Bi maana akamwacha aizungumzie.

Mtu aliye na msimamo wa dini kikweli basi anatakiwa kuwa na msimamo katika mambo yote yanayohusu dini na si katika baadhi ya mambo peke yake. Akiambiwa asizungumze basi aseme: “Dhambi zinakupata wewe.” Kuzungumza ni faradhi kwa baadhi ya watu na wako watu wanaotosheleza. Haina maana kwamba bwana huyu peke yake ndiye mwenye kuzungumza na hakuna mwingine zaidi yake anayeweza kuifikisha Shari´ah ya Allaah. Wako watu wengine. Akikubaliana na jambo hili na akaacha kuvutana basi pengine ikaja siku miongoni mwa siku akaruhusiwa kuzungumza. Huenda Allaah akawapa jambo hili wengine na wakamruhusu kuzungumza.

[1] 04:59

[2] 22:11

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa' al-Baab al-Maftuuh (10 B) Tarehe: 1413-05-04/1992-10-30
  • Imechapishwa: 10/03/2021